Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Manispaa ya Singida, kinatarajia kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi mbalimbali za uongozi ambazo zipo wazi, ikiwemo ya mwenyekiti wa wilaya, Mei, 14 mwaka huu.
Akizungumza na MO Blog, ofisini kwake jana, Katibu CHADEMA wilaya ya Singida mjini, Yahaya Ramadhani Hamisi, alisema zoezi la kuchuja wagombea limekamilika, na waliofanikiwa kuchaguliwa tayari wameshaanza kampeni ambazo zitamalizika Mei, 13 mwaka huu.
Alisema kwa nafasi ya mwenyekiti wa wilaya, wagombea ni Geofrey Irumba na Diwani wa viti maalumu, Josephine Lemoyani.
Yahaya alisema nafasi ya mwenyekiti wa wilaya ilikuwa wazi baada ya aliyekuwa madakarani, John Kalehe Kumalija (marehemu) kuondolewa kwa tuhuma ya kushindwa kumudu nafasi hiyo.
Aidha, alisema nafasi ya mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (BAWACHA) Manispaa ya Singida, inawaniwa na mgombea mmoja ambaye ni Christina Ntembo. Ntembo amewahi kuwa mwenyekiti wa UWT (CCM) wilaya ya Ikungi.
“Nafasi za katibu, mweka hazina, katibu mwenezi kwa upande wa BAWACHA kila nafasi inagombewa na mgombea mmoja mmoja ambao, ni Happines Shilla, Ester Mark na Sofia Hamisi. Nafasi ya umoja wa vijana, inagombea na Mohamed  Mwangu,” alisema katibu huyo.
Kwa upande wa nafasi za wajumbe wa BAWACHA, alisema zinagombewa na Rabeka Masasi, Rukia Dinawi, Salima Mrisho, Janne Gwau na Tausi Selemani. 
Katibu Yahaya , amewataka wagombea waendelea kufanya kampeni za kiustarabu na pia wajiandae kupokea matokeo ya kushinda au kushindwa.
Wakati huo huo,Katibu huyo alisema uchaguzi huo utasimamiwa na uongozi wa CHADEMA mkoa na utakuwa chini ya uangalizi wa uongozi CHADEMA kanda ya kati.
Na Nathaniel Limu, Singida