- Written by Nkupamah blog
Dodoma.
Harakati za wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), jana zilihamia katika ukumbi wa Bunge ambapo kila mmoja
wao alikuwa akitafuta
mbinu za kusalimiana na wabunge.
Hata
hivyo baadhi ya wagombea hao walikuwa wanatumia nafasi hiyo kuzunguka na
kuwafuata wabunge kwenye viti vyao, kiasi cha kufanya kuwepo na kile
Spika alichokita kama ni vurugu ndani ya Bunge.
Spika
Anne Makinda alilalamika mara kadhaa kuwa wabunge walikuwa wakifanya
vurugu ndani ya ukumbi na kuwataka watulie, kwani wengi walikuwa
wanapishana kwenye viti vya wagombea akiwamo Waziri wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Stephen Wasira ambaye kiti chake kilipata wageni wengi pia.
“Waheshimiwa
wabunge naombeni utulivu basi, mbona mnaleta vurugu kwa kutembea tembea
humu ndani wakati kanuni hazisemi hivyo, nitawataja kwa majina sasa,”
alisema Makinda.
Karibu
wagombea wote ambao ni wabunge, naibu mawaziri na mawaziri jana walikuwa
bungeni isipokuwa wagombea watatu wa CCM ambao ni Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala na Mbunge wa
Kisesa, Luhwaga Mpina ndiyo hawakuonekana.
Mapema
mgombea urais, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ndiye aliyekuwa wa
kwanza kuvunja mwiko baada ya kuhama katika kiti chake anachotumia kila
siku na kumfuata mgombea mwenzake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe na wawili hao walitumia muda mrefu wakizungumza pamoja.
Kutoka
hapo, Mwigulu alianza kuzunguka kwa staili yake kwa kwenda kwa wabunge
huku akiwa makini kwa kukwepa viti walivyokaa wagombea wenzake, ambao
wakati wote nao walikuwa na wabunge karibu yao wakizungumza.
Wagombea
wengine waliokaa pamoja kwa muda mrefu ndani ya ukumbi ni Waziri wa
Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri Mkuu Mizengo Pinda baada ya Magufuli
kumfuata Pinda katika kiti chake.
Mgombea
mwingine ambaye jana alionekana kutotulia katika kiti chake alikuwa ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya.(VICTOR)
Profesa
Mwandosya huwa hana tabia ya kuhama kiti chake na kuwafuata wabunge au
mawaziri na badala yake hufuatwa alipo, lakini jana hali ilikuwa
tofauti.
Profesa
Mwandosya alisalimiana na watu wengi ndani na nje ya ukumbi wa Bunge,
ambako alikutana na wabunge kadhaa wa Mkoa wa Mbeya akiwemo mgombea
mwenzake ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk
Harrison Mwakyembe na waliteta kwa muda.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa wabunge wengi kufika
kumsalimia anapokaa na haikuwa jambo geni jana, kwani ni kawaida yake
awapo ukumbini mara nyingi hukosa nafasi ya kupumua kutokana na msururu
wa wabunge.Hata hivyo, katika kiti ambacho wabunge hukitumia kuzungumza
naye, jana kilitumika zaidi na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM), Juma Sadifa ambaye alikaa kwa muda mrefu zaidi wakiteta na
alionekana kama ameziba nafasi ya wengine.
Nje ya
ukumbi wa Bunge, Dk Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe waliongoza kupata watu wengi waliokuwa
wakiweka msururu kuwasalimia.
Idadi
kama hiyo pia ilikuwa kwa Pinda, ambaye licha ya kuwa na ulinzi, lakini
nje ya ukumbi jana alisalimiana na watu wengi tofauti na siku zote.
Hata
hivyo Pinda tofauti na siku zote jana alikuwa na staili tofauti kwani
kila aliyemhisi kuwa alitaka kumpa walau mkono, alimfuata yeye na
kusalimiana jambo lililowapa wakati mgumu walinzi wake kumzuia.
Mgombea
pekee ambaye alikuwa na staili ya kwake katika salamu alikuwa ni Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye
toka ndani hadi nje alisalimia na watu wachache kwa kushikana mikono
huku akionekana kuwapungia mikono zaidi.CHANZO:MWANANCHI


0 comments :
Post a Comment