TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF) LEO


TAIFA STARS YAANZA MAZOEZI
KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kimeanza mazoezi katika uwanja wa Karume kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
Wachezaji wa Taifa Stars chini ya kocha wake mkuu Charles Mkwasa watakua wakijifua mara mbili kwa siku asubuhi na jioni katika uwanja wa Karume katika kujiweka fit na maandalizi ya mchezo huo.
Kufuatia baadhi ya wachezaji kuwa na majukumu na timu zao kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Hisani utakaochezwa Agosti 22, Mkwasa amewaongeza wachezji wengine kumi (10) kutoka katika orodha yake ya akiba.
Lengo la kambi hii ya awali ya siku tano, ni kocha mkuu pamoja na benchi lake la ufundi kupata nafasi ya kuwaona wachezaji katika mazoezi hayo kabla ya safari ya kuelekea nchini Uturuki Agosti 23 mwaka huu kwa kambi ya siku kumi.
Wachezaji walioitwa na kuanza mazoezi leo ni Said Mohamed, Vicent Andrew (Mtibwa Sugar), Mohamed Hussein, Ibrajim Hajibu (Simba SC), Hamis Ali, Juma Mbwana (KMKM), Tumba Sued (Coastal Unioni), Samuel Kamuntu (JKT Ruvu), Ibrahim Hilka (Zimamoto– Zanzibar) na Mohamed Yusuf (Prisons).
Wachezaji wengine waliopo kambini ni Said Ndemla, Hassan Isihaka, Abdi Banda(Simba SC), Rashid Mandawa (Mwadui FC), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Orgeness Mollel (Aspire Academy) na Abdulhaman Mbambi (Mafunzo).
TWIGA STARS KUIVAA HARAMBEE STARLETS
Timu ya Taifa ya  Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) iliyopo kambini kisiwani Zanzibar, inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya Wanawake kutoka Kenya (Harambee Starlets) Agosti 23, 2015.
Mchezo huo wa kirafiki utachezwa katika uwanja wa Aman Kisiwani Zanzibar, ikiwa ni sehmu ya maandalizi ya kikosi hicho kujiandaa na fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) zitakazofayika nchini Congo-Brazzavile kuanzia Septemba 4 – 19, 2015.
Twiga Stars inaendelea na mazoezi kutwa mara mbili katika viwanja vya Aman na Fuoni chini ya kocha wake mkuu Rogasian Kaijage kujiandaa na fainali hizo za michezo ya afrika, wachezaji wote waliopo kambini wapo katika hali nzuri wakiendelea kujifua na michezo ya Afrika.
USAJILI                                                                                         Dirisha la usajili limeongezwa toka tarehe 06 Agosti hadi tarehe 20 Septemba, baada ya muda huo klabu itakayochelewesha kuleta usajili wake itatozwa kiasi cha shilingi laki tano (Tsh 500,000) kwa kila mchezaji itakayemsajili mpaka siku ya tarehe 30 Agosti.
Mwisho wa kufanya uhamisho wa kimataifa wa wachezaji kwa njia ya mtandao TMS ni tarehe 6 Septemba.
Kikao cha kamati ya sheria kitakaa tarehe 28 kwa ajili ya kuupitisha usajili na kitakaa tena tarehe 8/9/2015 kwa ajili ya kupitisha usajili.
Kuanzia tarehe 21 hadi 27 itakuwa ni wiki ya pingamizi, ambapo majina yatabandikwa TFF Karume na kuwekwa kwenye mtandao ili kuwezesha vilabu vyenye pingamizi kuwawekea wachezaji mapingamizi.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kuanza tarehe 12 Septemba 2015, Daraja la kwanza (FDL) ikitarajiwa kuanza Septemba 17 na Ligi Daraja la pili inatarajiwa kuanza Oktoba 16 mwaka huu.
MICHUANO YA COPA COCA-COLA 2015
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) bado linaendelea na mazungumzo na wadhamini wa michuano hiyo (Coca-Cola). Kutokana na mazungumzo hayo, ratiba ya michuano hiyo itachelewa kutoka.
Hivyo, tunawaomba kuwa na uvumilivu wakati mchakato wa mazungumzo hayo yanayokaribia ukingoni ukiendelea.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment