Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema, Chiku Abwao
)kushoto) akiongea na wafuasi wa ACT - Wazalendo baada ya kupitishwa na
chama hicho kugombea ubunge Jimbo la Iringa Mjini. Picha na Said
Ngoamilo.
Dar/Iringa. Kada aliyewania ubunge kupitia Chadema
katika Jimbo la Kalenga na kutemwa kwenye kura za maoni, Mwanahamisi
Muyinga ameibuka mshindi wa kura hizo katika jimbo hilohilo kupitia
chama cha ACT-Wazalendo.
Katika uchaguzi uliofanyika katika Kata ya Mlandege mwishoni mwa wiki
iliyopita, Muyinga aliibuka mshindi kwa kupata kura 10 akifuatiwa na
Daniel Mwangili aliyepata kura saba, huku Edward Mtakimwa na Kiduo
Mgunga wakipata kura tatu kila mmoja.
Mbali na Muyinga, wengine waliotemwa Chadema na kushinda ACT ni
aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kunduchi, Janeth Rithe na Dickson Ngh’illy
aliyewahi kugombea Jimbo la Temeke mwaka 2010. Ofisa wa Habari wa ACT-
Wazalendo, Abdallah Khamis alisema jana kuwa Ngh’illy ameshinda katika
jimbo jipya la Kibamba baada ya kupata kura 19 kati ya 29
zilizopigwa. Alisema kabla ya kura hizo kupigwa,
mgombea mmoja alijitoa na kuacha nafasi hiyo ikiwaniwa na Ngh’illy,
Monalisa Ndala na Edna Mwango aliyeambulia kura mbili. “Rithe ameshinda
baada ya kupata kura 38 kati ya 58 Jimbo la Kawe, huku Mohamed Ngulangwa
akiibuka kidedea Jimbo la Temeke baada ya kupata kura 80 kati ya 93,”
alisema Khamis.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Muyinga aliwashukukuru
wapigakura na wakazi wa Kalenga kwa kumuamini na kumpa fursa ya
kupeperusha bendera ya chama hicho na kwamba hatawaangusha.
“Nawashukuru kwa kunipa heshima hii. Nataka kuwaeleza kuwa mimi natoka
ukoo wa machifu, nimeomba ruhusa ya kuifanya kazi hii katika Jimbo la
Kalenga na nimeruhusiwa,” alisema Muyinga na kuongeza:
“Nawafahamu wakazi wa Kalenga kwa zaidi ya asilimia ya 90. Najua kuwa
wanategemea kilimo na mimi nimesoma mambo ya kilimo, nitatumia taaluma
yangu kuwaletea maendeleo.”
0 comments :
Post a Comment