Aliyekuwa
naibu wa kiongozi wa waasi wa Lords Resistance Army LRA nchini Uganda,
Dominic Ongwen, anafikishwa kizimbani katika mahakama ya Kimataifa ya
Uhalifu ya ICC. Ongwen alikuwa msaidizi wa kamanda wa LRA Joseph Kony
Dominic
Ongwen atafikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa inayoshughulikia
uhalifu yenye
makao yake mjini The Hague, Uholanzi, akituhumiwa kuhusika
na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Upande wa mashitaka
unatumai kupata taarifa zaidi kuhusu mfumo wa uongozi wa kundi hilo
wakati wa kesi hiyo ya Ongwen.
Ongwen
alitekwa nyara na LRA akiwa na umri wa miaka kumi alipokuwa akielekea
shuleni na kulazimishwa kuwa mpiganaji wa kundi hilo. Alijipatia
umaarufu na kuheshimika katika kundi hilo LRA kwa kufanya mauaji ya
kinyama, kupora mali na kubaka kama mfuasi sugu wa Kony na kupandishwa
cheo hadi kuwa naibu wa Kony.
Mnamo
mwezi Januari mwaka huu, alijisalimisha kwa kikosi maalumu cha jeshi la
Marekani waliokuwa wanashiriki katika operesheni ya kumtafuta Kony
katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kukabidhiwa kwa ICC.
Ongwen ni muathiriwa au mtuhumiwa?(P.T)
Kesi
dhidi yake itafuatiliwa kwa makini kwa sababu huenda ikaangazia suali la
je ni muathiriwa wa uasi wa LRA au ni mtuhumiwa? ICC iliamua kuwa
watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambao wametekwa nyara au kuhusika
katika uhalifu wa kivita wachukulike kama waathiriwa.
Licha ya
kuwa Ongwen alikuwa na miaka kumi alipotekwa nyara na LRA, kipindi cha
kujisalimisha kwake alikuwa na miaka 32. Ni uamuzi wa mahakama sasa
kuamua iwapo anapaswa kutuhumiwa kwa uhalifu alioutenda na ni kwa kiasi
gani.
Mwaka
2005, mahakama ya ICC ilitoa kibali cha kukamatwa kwa Kony mwenye umri
wa miaka 55 aliyeanzisha LRA mwaka 1986 baada ya kudai kupokea maagizo
kutoka kwa Roho Mtakatifu ya kuunda Dola la Kikiristo Uganda kuambatana
na Bibilia na amri kumi za Mungu.
Kiongozi
wa LRA Joseph Kony au kama anavyojulikana kwa jina la 'Mchinjaji wa
Uganda' anasemekana kuwateka nyara zaidi ya watoto 7,000. Kundi lake la
LRA linawatumia watoto hao kama wapiganaji na watoto wa kike kama
watumwa wa ngono.
LRA imefanya vitendo vya kikatili
Ili
kuwazuia wavulana kutoroka kutoka kundi hilo na kurejea vijini mwao,
wengi wa watoto hao wanalazimishwa kuwaua mama zao. Wanawake na
wasichana wanabakwa na kulazimishwa kuwaoa wapiganaji.
Waasi hao
wa LRA wamevishambulia vijiji, kuwatesa raia kaskazini mwa Uganda na
kuwaua takriban watu laki moja tangu walipoanzisha uasi, huku zaidi ya
watu milioni mbili wakilazimika kuyatoroka makaazi yao kutokana na mzozo
huo.
Lakini
mpaka sasa kiongozi huyo waasi ameweza kukwepa mkono wa sheria
akiaminika kuwa katika eneo la mpakani aidha, Jamhuri ya Afrika ya Kati,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan au Sudan Kusini.
Chanzo:DW


0 comments :
Post a Comment