Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe
Magufuli jana tarehe 23 Januari, 2016 ametunuku kamisheni kwa Maafisa
wapya 205 wa jeshi la wananchi kundi la 57/15 katika Chuo cha mafunzo ya
kijeshi (TMA) Monduli Mkoani Arusha.
Maafisa hao wapya wametunukiwa cheo cha Luteni Usu, ambapo kati yao 16 ni maafisa wanawake, na 189 ni maafisa wanaume.
Aidha,
miongoni mwa maafisa wapya 205 waliotunukiwa kamisheni, maafisa 10
wametoka majeshi rafiki kutoka nchi za Uganda, Kenya na Burundi.
Akiwa
katika uwanja wa paredi wa chuo hicho Rais Magufuli amepokea heshima
zote za kijeshi ikiwemo kupigiwa wimbo wa Taifa na kukagua gwaride rasmi
lililojumuisha maafisa hao wapya.
Baada
ya kutunukiwa kamisheni, Maafisa wapya wa jeshi wamekula kiapo na
wametoa heshima kwa gwaride lililopita mbele ya Rais kwa mwendo wa pole
na mwendo wa haraka.
Viongozi
wengine waliokuwepo katika tukio hilo ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
Ombeni Sefue, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange,
Maafisa wa ngazi za juu jeshini na Maafisa wastaafu, viongozi wa mkoa na
wilaya na wakufunzi kutoka nje ya nchi.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kutoa kamisheni kwa Maafisa wapya
wa Jeshi la wananchi tangu achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mwezi Oktoba Mwaka jana.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha.
23 Januari, 2016.
0 comments :
Post a Comment