Chama cha Watu Wenye Ualbino
Tanzania (TAS) wameiomba Serikali kuwasaidia kumtafuta Bw. Said Abdalah
Ismail (47) mkazi wa Kijiji cha Mbezi Mlungwana Wilaya ya Mkuranga
mkoani Pwani.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
salaam na Kaimu Katibu Mkuu wa (TAS) Josephat Torner alipokua akiongea
na waandishi wa habari juu ya taarifa hii ya kupotelewa na mwenzao.
“TAS kwa kushirikiana na Shirika
la Under The Same Sun (UTSS) tunaendelea kufanya juhudi ya kumtafuta na
juhidi zetu tunaomba Serikali ituunge mkono” alisema Torner
Torner aliongeza kuwa, Said
alionekana kwa mara ya mwisho Januari 31 mwaka huu katika Kijiji cha
Mtipule alikokwenda kuuza mboga za majani na baadae alionekana katika
kilabu cha pombe ya kienyeji ambapo inasemekana aligombana na wenzie
waliokua wakinywa pamoja kabla hajaondoka kilabuni hapo.
“Tunalitaka Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na lile la Afrika Mashariki kujadili kwa kina
tatizo hili na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu pia vyombo vya dola
kuhakikisha wakatili hao wanatafutwa, wanakamatwa na kufikishwa mbele ya
sheria ili sisi wenye ualbino tuweze kuishi kwa amani.” Alisema
Torner.
Amesema kuwa pamoja na juhudi za
kumtafuta Said kuendelea taarifa ya kupotea kwake ilipelekwa kituo cha
Polisi Wilaya ya Mkuranga na kupewa RB namba MKU/PE/05/2016 pia kituo
kidogo cha polisi Kimanzichana kwa RB namba KIM/RB/50/2016.
Aidha, Polisi wanaendelea na
uchunguzi kuhusu tukio hilo ambapo jina la muuza pombe pamoja na majina
ya wale aliogombana nao tayari yamewasilishwa polisi kwa ajili ya
uchunguzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
chama cha Albino wilayani Mkuranga mkoani Pwani Hassan Kambangwa
akizungumzia tukio amesema amelipokea kwa masikitiko makubwa na kuiomba
Serikali kuwachukua hatua kali za kisheria wote waliohusika katika tukio
hilo.
Kambangwa ametoa wito kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji kutafuta mbinu za kuzuia ukatili huo.
Ikumbukwe kuwa tukio hilo kwa
Bw.Said Abdalah Ismail ni la pili kwa kuwa aliwahi kupatwa na mkasa wa
kukatwa kiganja cha mkono akiwa mkoani Morogoro miaka michache
iliyopita.
0 comments :
Post a Comment