Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF) leo imefungua kesi namba 23 ya mwaka 2016 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,George Mcheche Masaju, Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na waliokuwa wanachama wa chama hicho wapatao 11.
Wakili wa Mahakama Kuu na Mwanasheria wa CUF, Hashimu Bakari Mzirai wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua kesi hiyo, amesema Bodi ya Wadhamini ya CUF imeifungua kesi hiyo kwa hati ya dharula kwa lengo la kusikilizwa kwa haraka ili mahakama itoe maamuzi mapema.
“Kuhusiana na kesi tuliyoahidi watanzania kuwa chama kinaenda kuifungua dhidi ya msajili wa vyama vya siasa, mwanasheria mkuu wa serikali, Lipumba na wanachama waliokiasi chama,” amesema. Ameongeza kuwa “Kesi hii imefunguliwa leo na jopo la mawalili wa CUF, imeletwa kwa hati ya dharula, imesajiliwa na tutawapa maelezo zaidi hapo baadae sababu kesi itapangwa kwa jaji muda si mrefu,”
Mziray amedai kuwa, katika kesi hiyo, bodi imeiomba mahakama kuu mambo matatu, kwanza kutengua barua ya Septemba 23, 2016 kutoka kwa Jaji Mutungi aliyodai kuwa ililenga kutengua maamuzi halali ya vikao vya chama hicho kutokana kwamba barua hiyo ilieleza kuwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa inamtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho.
Pili, kumzuia Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia maamuzi ya chama hicho ya kumfuta uanachama Lipumba kwa madai kuwa chama hicho kupitia Baraza Kuu la Uongozi kimemfuta uanachama.
Jambo la mwisho, Mziray amedai kuwa, bodi hiyo pamoja na viongozi wa CUF, inataka kufanya siasa na kwamba inaona msajili ndiyo kikwazo cha shughuli zake hususan za kisiasa za chama hicho ambapo imeitaka mahakama imzuie kuingilia masuala ya CUF na kuingilia maamuzi ya vikao halali vya chama.
Mziray ameeleza kuwa “Hati ya darura hutoeka pale kunapokuwa na jambo la hatari nadhani mnafahamu kwamba ofisi kuu ya chama imeshimiliwa na watu, na kwamba imefungua kesi kwa hati ya dharula ili iweze kudhibiti ofisi zake hasa ofisi kuu iliyopo buguruni.Jambo la pili wanachama wanashauku ya kujua hatma ya chama chao nashukuru kwamba mahakama ina spidi ya kusikiliza kesi hivyo wanachama watafahamu hatma ya chama chao hivi karibuni,”