Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amemshukia Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai na kumtaka kuacha unafiki kuhusu futari yake aliyoandaa na kususiwa na wabunge wa upinzani.
Lissu amesema kuwa hawezi kushiriki kwenye futari ya Spika Ndugai au kiongozi yeyete wa CCM kwa sababu wameamua kuwabagua na kuwadhalilisha.
Maneno hayo ya Lissu yamekuja ikiwa ni siku chache tangu Spika Ndugai alipoeleza kuhusu madai ya upinzani kupanga kususia futari yake aliyoandaa Jumanne wiki hii na kusema kuwa jambo hilo si zuri kwani kuna umuhimu wa jamii kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao.
Ndugai alielezea pia wabunge wa upinzani walisusia futari iliyokuwa imeandaliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisema kuwa, inapofikia hatua ya kutoshirikiana katika masuala ya kijamii inakuwa sio vizuri sana.
Lissu alisema kuwa kiongozi huyo amekuwa akiwadhalilisha na kutoa adhabu za vifungo vya nje ya bunge huku akiwazuia kutoa mawazo mbadala ndani ya bunge.
“Kiongozi anayewabagua namna hii bungeni, unawezaje kwenda kwenye futari au shughuli yake? Aache unafiki kwa lengo la kutaka kuonekana mwema machoni mwa jamii.”
Aidha, Lissu alienda mbali na kusema kuwa Ndugai amebinafsisha shughuli za bunge kwa serikali na kwamba kwa sasa anafanyakazi kwa kushirikiana na serikali badala ya bunge kubaki lifanye shughuli za kibunge.
0 comments :
Post a Comment