Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa Bi. Asma Juma (29) aliyedai kuibiwa mtoto mmoja kati ya mapacha katika hospitali ya Temeke taarifa inaonyesha hakuwa na watoto pacha ila alikuwa na mtoto mmoja.
Waziri Ummy ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa tume huru Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama, Dkt. Charles Majige aliyoiunda kwaajili ya kuchunguza sakata hilo.
“Nimepokea taarifa kutoka kwa tume huru niliyoiunda hivi karibuni na imethibitisha kuwa Bi. Asma Juma hakuwa na watoto mapacha ila uchukuaji mbaya wa picha ya mtoto aliyekuwa tumboni uliofanywa katika zahanati ya Huruma ukatoa matokeo hayo,” alisema Waziri Ummy.
Hata hivyo Waziri Ummy amesisiitiza kuwa wanafamilia ya Bi. Asma wanatakiwa kumfariji ndugu yao na sio kumkumbushia jambo hili mara kwa mara kwani litamharibu kisaikolojia na kushindwa kutekeleza wajibu wake kwa mtoto kama mama mzazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt. Charles Majige amesema Bi. Asma aliamini hivyo kwa sababu hospitali ya Temeke hawakumchukua vipimo vya picha bali walitumia taarifa ya vipimo vya awali.