Rais
Jakaya Kikwete alibadili upepo wa mchakato mzima wa Katiba baada ya
kutoa maoni yake binafsi, akitaka muundo wa Serikali mbili badala
ya
tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza
katika ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete
alipangua hoja moja baada ya nyingine zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume
hiyo, Jaji Joseph Warioba wakati akiwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni
Machi 18, mwaka huu.
Katika
hotuba yake hiyo ya saa 2:49 iliyokuwa na maneno ya 'kuuma na kupuliza'
kuhusu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba, Rais Kikwete alisema suala la
muundo wa Muungano ndiyo ajenda mama katika Rasimu ya Katiba na kwamba
iwapo wajumbe watatoa uamuzi usio sahihi, nchi inaweza kujaa migogoro
ambayo haikuwapo.
Huku
akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo, Kikwete alisema kuwa wanaotaka
Serikali tatu waangalie changamoto zake na kuzitafutia majibu, kwa
maelezo kuwa muundo huo unaweza kuvunjika kirahisi.
Alisema
ingawa Jaji Warioba aliwatoa hofu wananchi kuwa Serikali tatu hazitakuwa
na gharama kubwa, ukweli ni kwamba muundo huo una gharama na
utekelezaji wake ni mgumu na kusisitiza kuwa CCM inaweza kuzimaliza kero
za Muungano bila kuhitaji uwapo wa Serikali ya tatu.(P.T)
Huku
akichambua kile kilichoelezwa na Jaji Warioba sambamba na kuwapiga
vijembe wenyeviti wa vyama vya upinzani akiwamo Christopher Mtikila (DP)
na Freeman Mbowe (Chadema), Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu;
"Sababu
ya kwanza ni kwamba muundo huo ndiyo matakwa ya Watanzania wengi Bara na
Zanzibar. Sababu ya pili muundo huo unatoa majibu ya uhakika na
endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili
zinazolalamikiwa na pande zote mbili."
Aliongeza,
"Wapo wanaokubaliana na tume na kwamba muundo wa Serikali tatu ni
matakwa ya wengi na hauepukiki na kwa msemo wa Kiswahili wengi wape.
Lakini wapo wanaopingana na takwimu za tume kwamba hazionyeshi ukweli
huo. Mimi nasema maneno yanayosemwa na watu siyo yangu." Huku
akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo alisema, "Watu wanasema
Watanzania waliotoa maoni kwa tume ni 351,664, kati yao 47,820 sawa na
asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano. Watu 303,844 sawa
na asilimia 86.4 hawakuwa na tatizo na muundo wa Muungano na wala
hawakuuzungumzia wakati wa kutoa maoni."
Alisema
hivi sasa watu wanahoji iweje asilimia 13.6 ndiyo wageuke Watanzania
walio wengi ambao wametoa maoni ya kutaka Serikali tatu.
"Watu
wanahoji mbona taarifa ya tume inayohusu takwimu (ukurasa 66,67),
inaonyesha kati ya watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu muungano watu
17,280 ndiyo waliotaka Serikali tatu ambao ni sawa na asilimia 37.2 na
waliotaka muundo wa Serikali mbili ni asilimia 29.8, Serikali ya mkataba
asilimia 25.3 na Serikali moja asilimia 7.7" alisema. Alisema taarifa
ya tume inaonyesha kuwa watu 772,211 waliotoa maoni ni asilimia 10.4
ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6
hawakuzungumzia Muungano, bali mambo mengine.
"Watu
wanahoji kama Muungano ni jambo linalowakera sana Watanzania
ingethibitika kwenye wingi wa wale waliotoa hoja. Usahihi wa hoja hii ni
upi, nawaachie nyie (wajumbe) mjadili" alisema huku akishangiliwa kwa
nguvu.
Akizungumzia
sababu ya pili ya tume kwamba muundo wa Serikali tatu unajibu
changamoto za muundo wa Serikali mbili, huku akifafanua kero
zinazotolewa na kila upande wa Muungano alisema; "Nyinyi ndiyo waamuzi,
sikilizeni vizuri hoja hizi mtafakari na kuamua. Tume yenyewe imekiri
kuwa muundo wa Serikali wa Serikali tatu una changamoto zake ikiwa ni
pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma."
Alisema
wajumbe wa Bunge hilo wanatakiwa kutafuta majibu mwafaka kuhusu
changamoto za muundo wa Serikali tatu kwa sababu maelezo ya tume kuhusu
muundo huo hayana majibu.
Aliongeza,
"Kupanga ni kuchagua. Wanaounga mkono Serikali mbili wanasema mlolongo
wa changamoto ulioanishwa na tume kuhusu Serikali tatu hautapunguza
matatizo bali utayaongeza kuliko ilivyo sasa na wanasema changamoto hizo
zinatatulika bila kuwepo Serikali ya tatu."
Alisema
kama mfumo wa Serikali tatu ukipita ni lazima Serikali ya tatu ijengewe
msingi imara kwa sababu haitakuwa na chanzo cha uhakika cha mapato yake
yatakayoiwezesha kusimama yenyewe na haitakuwa na chombo cha kukusanya
mapato zaidi ya kutegemea kukusanyiwa mapato na nchi washirika.
"Kama
tunataka Serikali ya tatu lazima tuitengenezee misingi ya uhakika. Hivi
nani atakudhamini kwa virungu, pingu, magari ya kuwasha, majeshi au
bunduki. Serikali hii ya tatu haidhaminiki wala kukopesheka," alisema
huku akitolea mfano jinsi mataifa kama Urusi yalivyoanguka baada ya
kujitenga.
Huku
akifafanua jinsi kero za muungano zilivyotatuliwa na kamati na tume
mbalimbali mpaka kubaki kero sita, Rais Kikwete alisema Serikali ya
Muungano na ile ya Zanzibar zimeamua kutumia mchakato wa Katiba
kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Alisema
wakati Tanganyika na Zanzibar zinaungana kulikuwa na mambo 11 ya
muungano, baadaye kuongezeka hadi mambo 22 na kusisitiza kuwa mambo
mengi yaliibuka baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka
1977.
Alisema jambo ambalo Serikali hizo mbili walikubaliana kuliondoa katika mambo ya Muungano ni suala la gesi asilia na mafuta.
Ammwagia sifa Warioba
Alisema
Jaji Warioba wa wajumbe wenzake wa Tume ya Katiba wameandika Rasimu ya
Katiba vizuri na kwa weledi wa hali ya juu, na kwamba wametoa maoni
ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba tuliyonayo sasa.
"Katiba
inayopendekezwa imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda
vyema na wakati tuliokuwa nao na kuweka misingi mizuri kwa huko mbele
tuendako," alisema.
Alisema
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi kina
kurasa 106, sura 17, hivyo wajumbe wa Bunge la Katiba wanapaswa kusoma
kila kitu na kuelewa na kuamua kwa utashi wao.
"Uamuzi
wako siyo uamuzi wa kuambiwa na mwenzako, unaulizwa na wenzako kwenye
hilo tusemeje unasema na mimi nimeambiwa, ebo! Umeambiwa, umefundishwa
na mimi nasema akili za kuambiwa..." alisema Rais Kikwete.
Mambo mengine
Pia Rais
Kikwete aligusia suala la mbunge kupoteza ubunge iwapo atashindwa
kufanya kazi kwa miezi sita mfululizo, kutokana na maradhi au kizuizi
ndani ya gereza.
Alisema
anaungana na wote wanasema jambo hilo liangaliwe vizuri na kwamba
anashauri kama akiwa kizuizi amepatikana na makosa apelekwe mahakamani.
"Kwa
mazoea ya duania ukomo unawekwa kwa wakuu wa nchi, hawaweki ukomo kwa
wabunge, Tanzania wanataka kuwa wa kwanza," alisema Kikwete.
Kuhusu
suala la ugonjwa alisema mbunge anaweza kupata ajali akiwatumikia
wananchi wake, hivyo siyo sahihi kumwekea mgonjwa muda maalumu wa kuugua
kwake.
Huku
akicheka, Rais Kikwete alisema kitendo hicho kitawafanya wabunge kuanza
kutembea na dripu katika majimbo yao kabla hawajapona vizuri.
Chanzo:Mwananchi
0 comments :
Post a Comment