Wednesday, May 30, 2012
UFAFANUZI
WA MAMBO MBALIMBALI YALIYOPOTOSHWA NA MHE. ZITTO ZUBERI KABWE – NAIBU
KATIBU MKUU WA CHADEMA KATIKA HOTUBA YAKE ALIYOITOA KWA WATANZANIA
WAISHIO NCHINI MAREKANI
1. KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Katika
hotuba yake anadai kwamba mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa
unatokana na shinikizo la CHADEMA, Asasi za kiraia na viongozi wa dini.
UFAFANUZI
Huo
ni upotoshaji mkubwa na wa wazi kabisa unaolenga kufuta historia sahihi
ya mchakato wa uandikaji au upatikanaji wa Katiba Mpya unaoendelea hivi
sasa.
Ni
jambo lililo dhahiri kabisa kwamba mchakato wa Katiba Mpya ni
utekelezaji wa hotuba ya Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
aliyoitoa katika salamu za kuaga mwaka 2010 kukaribisha mwaka 2011 na
baadaye katika sherehe za Chama Cha Mapinduzi kutimiza miaka 34 Mjini
Dodoma. Hili ndilo chimbuko halisi la hoja ya Katiba Mpya.
Akitoa
maamuzi hayo alisema Katiba iliyopo sasa ni nzuri, imetuvusha salama
miaka hamsini iliyopita, tukiwa wamoja, imetujengea umoja wa Kitaifa. Lakini
katika kipindi hicho hicho kumetokea mabadiliko mengi duniani na hapa
nchini ya kisayansi, kiteknolojia, kitamaduni, kisiasa n.k. Hakuna shaka kwamba sasa tunahitaji Katiba Mpya itakayotuvusha miaka mingine 50 ijayo. Jambo hili Zitto Kabwe kalinukuu kwenye hotuba yake anaposema kuwa:-
“Tanzania
tunayoitaka kwa miaka mingine hamsini ….” Mantiki hii ya miaka mingine
50 inatokana na hotuba ya Mhe. Dr. Jakaya M. Kikwete sio yeye.
2. KUHUSU UBADHIRIFU SERIKALINI
Katika
hotuba yake amedai kuwa CHADEMA ndio viongozi waliobeba dhamana ya
mpito huu, kutoka Serikali ya kibadhirifu isiyojali watu mpaka Taifa
lenye demokrasia iliyokomaa na lenye maendeleo na ustawi wa watu wake. (Developmental Democratic State).
UFAFANUZI
Kwanza CHADEMA haina “dhamana”
ya uongozi wa nchi, mwenye dhamana ya uongozi wa nchi ni Chama Cha
Mapinduzi ambacho kina Rais ambaye ni Mkuu wa nchi, Mkuu wa Serikali na
Amiri Jeshi Mkuu. CHADEMA
wanachokitafuta ni Mob leadership ambayo ni fujo “Anarchy or law
lessness” kitu ambacho huwezi kukidhibiti hata ukishika madaraka (mfano
ni Libya, Mali, Algeria n.k.).
Mob
leadership ni fujo kwa sababu ina watu ambao hawana sera ya pamoja
hawana wajibu wa kisheria, hawana maslahi ya kijamii na kidini, wanadai
haki bila wajibu.
Dhamana
ya kuwafikisha watu katika Serikali ya kidemokrasia imo mikononi mwa
Serikali iliyopo madarakani. Matamshi yanayotolewa na baadhi ya viongozi
wa CHADEMA yanaonyesha dhahiri kuwa hawathamini demokrasia ya nchi,
umoja wa kitaifa wala amani na utulivu.
Mfano:-
(i) Tamko la Mhe. Joshua Nassari la kumzuia Rais, Mkuu wa Nchi, asikanyage Mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania.
(ii) Tamko la Mhe. Kabwe la kudai kuwa Wazanzibar wameporwa mafuta na gesi.
(iii) Hata
kwenye uchaguzi mdogo wa Mbeya vijijini mwaka 2009 CHADEMA ilitamka
kwamba Mhe. Ali Hassan Mwinyi Rais Mstaafu asikanyage Mbeya.
(iv) Tamko
la Mhe. Wenje kuwa Mwanza inajitosheleza kuwa nchi kwa rasilimali zake
na hivyo kupendekeza serikali za majimbo ili Mwanza ijiendeshe yenyewe.
Matamko
haya hayawezi kutamkwa na kiongozi mmoja wa CHADEMA bila ridhaa ya
Chama ama sivyo wangekuwa wanachukuliwa hatua na Chama chao.
Kwa
kuwa matamshi haya ni uhaini, uchochezi na ufashisti (ANARCHY). Kauli
hizi zinaweza kupelekea machafuko katika nchi, mgawanyiko, ubaguzi, fujo
na umwagaji damu, mambo ambayo yatamwathiri kila raia wa Tanzania bila
kujali Chama chake cha kisiasa.
Kwa
hiyo, Chama Cha Mapinduzi ambacho kina dhamana ya uongozi wa nchi hii
kinalaani matamshi hayo na kinawataka viongozi wa vyama vya siasa waache
kutoa matamshi ya hovyo na hatari kwa mstakabali wa Taifa letu. Chama Cha Mapinduzi kinaitaka Serikali kufuatilia matamshi haya kwa kina na itoe taarifa kwa wananchi.
3. KUHUSU WATANZANIA KUTAKA UONGOZI MPYA
Katika utangulizi wa hotuba yake amedai kuwa “watanzania
kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu wameamka na
kutaka mabadiliko ya kisiasa na hasa kutaka kabisa uongozi mpya wa nchi
kutoka Chama kingine tofauti na Chama kinachoongoza hivi sasa.”
UFAFANUZI
Chama
kinachoongoza hivi sasa ni Chama Cha Mapinduzi “CCM” unapozungumza
kauli kama hii lazima uangalie na hali halisi ya Chama chenyewe kama
Taasisi.
Kwanza, Chama Cha Mapinduzi kina wanachama hai wengi ambao ni watanzania kuliko CHADEMA.
Pili, Chama Cha Mapinduzi kina mashabiki na wapenzi wastaarabu ambao ni watanzania wengi kuliko CHADEMA.
Tatu,
Chama Cha Mapinduzi katika mfumo wake hakijapata ombwe la uongozi, kina
uongozi katika ngazi za Shina, Tawi, Kata, Jimbo, Wilaya, Mkoa na Taifa
na hao wote ni watanzania. Na kama kuna Chama chenye heshima ya kuwasemea watanzania wote kila kona ni CCM sio Chama kingine chochote.
Nne,
katika uchaguzi wa ndani ya Chama wa mwaka 2012, watanzania wameendelea
kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi ndani ya CCM. Mpaka sasa Mashina yamekwishafanya uchaguzi kwa asilimia 97.56. Hao walioshiriki uchaguzi huo wa mashina ni watanzania.
Tano, katika chaguzi ndogo za Kata, Vijiji, Mitaa na Vitongoji CCM imeendelea kuongoza na wanaopiga kura nao ni wantanzania.
Sita,
Chama Cha Mapinduzi tangu 2007 kimefanikiwa kufungua matawi yake nje ya
nchi maeneo mbalimbali mfano India, Uingereza na Marekani. Hao
ni watanzania waishio katika ulimwengu wa kwanza na wanaamini kuwa CCM
bado ni imara na hata Mhe. Rais alipoalikwa juzi kuhudhuria mkutano wa
G8 alikutana na wanachama wa CCM Tawi la Marekani. Kitendo cha Mhe. Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kualikwa G8 ni heshima kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa
kuwa kigezo cha kumwalika kilikuwa ni demokrasia, utawala bora, amani
na utulivu nchini vigezo ambavyo vinavutia wawekezaji kutoka nje.
Kwa hiyo, hoja ya Mhe. Zitto ni Batili (futile) kwa sababu anatazama kwa macho ya ubinafsi kwa lengo la kugombea Urais mwaka 2015.
Uongozi mpya kabisa wa nchi ni upi? Kwa
kuwa uongozi wa nchi yoyote huru na ya kidemokrasia unapatikana kwa
utaratibu wa uchaguzi wa kawaida unaozingatia Katiba na Sheria za nchi
katika mazingira ya uhuru na uwazi na vyama vyote vinashiriki. Afafanue
maana ya uongozi mpya kabisa na namna utakavyopatikana huku akijua
kabisa kwamba vyama vyote vya siasa vitakuwa na haki ya kushiriki
uchaguzi. Lazima utapata uongozi mchanganyiko kama ilivyo hivi sasa katika mfumo huu wa vyama vingi.
4. KUHUSU SERA YA MADINI YA 2009 NA SHERIA YA MADINI YA 2010
Katika
hotuba yake amedai kuwa Tanzania haina sera ya Gesi asili na kwamba,
sheria ya madini ya mwaka 2010 imetokana na shinikizo la CHADEMA na
Asasi za kiraia.
UFAFANUZI
Chama Cha Mapinduzi katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo inapatikana katika website ya CCM www.ccm.or.tz
katika ibara ya 55 ya ilani imeeleza mafanikio yaliyopatikana katika
sekta ya madini kwa kipindi cha 2005/2010, ambayo ni pamoja na
kukamilika kwa sera ya madini ya 2009 na kupitishwa kwa sheria ya madini
ya mwaka 2010.
Mhe. Kabwe mwaka 2009 alikuwa wapi kutoa mchango wake?
Hoja hii ni ya CCM yeye na Chama chake wameidandia kwa malengo ya kibinafsi na sio maslahi ya nchi.
5. SUALA LA URAIA WA NCHI MBILI (DUAL CITIZENSHIP)
Mhe. Zitto anadai kwamba suala la uraia wa nchi mbili ni sera ya CHADEMA.
UFAFANUZI
Suala
la uraia wa nchi mbili limekuwa ni sera ya Chama Cha Mapinduzi na
limesimamiwa na Serikali yake, hususan Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe.
Katika
hotuba ya bajeti ya 2011/2012 iliyotolewa na Mhe. Bernard Membe Bungeni
katika Bunge la Nne kikao cha 31 cha tarehe 22 Julai, 2011 alisema:-
“Ni
dhamira ya Wizara yangu kuona suala la uraia wa nchi mbili
linazinduliwa sanjari na Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.”
Watanzania
mnapaswa kujua jinsi Zitto Kabwe anavyoiba hoja kwa manufaa binafsi
alipowadanganya watanzania waishio nchini Marekani na dunia kwa ujumla
akisema:-
“CHADEMA inataka suala hili lifikie mwisho kwenye mjadala wa Katiba.”
Huo
ni uwongo mkubwa na uzushi, kwa kuwa dhamira hiyo ni ya Serikali ya CCM
na ilishawasilishwa na Waziri mwenye dhamana Bungeni na yeye akiwepo.
6. HALI YA UCHUMI WA NCHI
Amedai
kuwa uchumi unaokuwa hivi sasa sio uchumi wa watanzania bali ni uchumi
wa watu wachache kwenye sekta chache kama madini, mawasiliano na ujenzi;
hivyo kupelekea watanzania wengi zaidi ya 15m kuishi chini ya Tshs. 500
kwa siku, kutokuwa na uhakika wa kula na kukabiliwa na mfumuko wa bei.
UFAFANUZI
Kwanza, takwimu zake sio za kitafiti kwani hazionyeshi chanzo. Pili
hazina ulinganisho wa hali ya maisha ya wananchi wa nchi
zinazotuzunguka ili uchungu alionao moyoni uonekane waziwazi kama ni
kweli au ni uzushi.
Mhe.
Kabwe amepotosha kwa makusudi ya kulinda maslahi binafsi ya Urais wa
2015 kwa kuwa haiingii akilini kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama takwimu
hizo yeye hajazisoma.
Kwa
mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2010
kilichotolewa na Wizara ya Fedha kukuwa kwa sekta ya kilimo kumeongezeka
kwa 4.2% mwaka 2010 tofauti na asilimia 3.2% mwaka 2009. Lakini katika taarifa yake anadai kuwa uchumi wa vijijini ambako ndiko kwenye kilimo umekuwa kwa asilimia moja tu (flat lining).
Katika
uchambuzi wake wa hali ngumu ya uchumi na mfumuko wa bei kama
angelinganisha na nchi jirani angegundua kuwa mfumuko wa bei kwa
Tanzania upo chini zaidi kwa asilimia 19 ukilinganisha na nchi
zinazotuzunguka ambao mfumuko ni mkubwa zaidi mfano Ethiopia ni 30%.
Katika
hali halisi ya maisha ya watanzania wa vijijini chakula chao hakitokani
na pesa, wanakula vitu vingi ambavyo haviingii kwenye takwimu za uchumi
mfano, kuku, mayai, maziwa, mihogo, viazi vitamu, nyama n.k. Hivyo vinaliwa bila kuingia kwenye mzunguko wa soko ndio maana hakuna mtanzania anayekufa njaa. Lakini nchi jirani wanakufa njaa na wanakimbia nchi zao kwa njaa. Mfumuko wa bei ni tatizo la Dunia nzima sio Tanzania peke yake.
Huyu
ni mgombea Urais wa aina gani ambaye si mkweli kwa nchi yake, hasomi
takwimu na anaropoka mambo ya ndani ya nchi hovyo hovyo duniani.
7. SUALA LA FURSA YA ELIMU
Katika
hotuba yake ameeleza kuwa “leo mtoto wa maskini Tanzania hapati elimu
anayopata mtoto wa mwenye uwezo.” Na kwamba Tanzania ijiandae kupokea
bomu litakaloletwa na kundi kubwa la vijana wasio na elimu wala ujuzi.”
UFAFANUZI
Huo ni uwongo na uzushi unaolenga kutetea maslahi binafsi. Kwa
kuwa katika uchambuzi wake amejikita kwenye shule binafsi na sio shule
za serikali ambazo zipo katika vijiji vyote Tanzania, vinatoa elimu
huru, sawa na bila ubaguzi.
Serikali ya Tanzania imetoa fursa ya Elimu kwa kila mtoto wa Tanzania tangu awali. Mpaka imefikia wakati hata mabinti wa kazi za ndani (house girls) hawapatikani wote wapo mashuleni.
Kuthibitisha
hilo mnamo tarehe 20/9/2010 Tanzania ilipata tuzo ya utekelezaji mzuri
wa miradi ya Elimu katika ngazi za awali, elimu ya msingi na sekondari
kutoka umoja wa mataifa. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokea Tuzo hizo Mjini New York.
Hivi
huyu Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA anakuwa wapi asiyaone haya mpaka
kwenda kuwadanganya watanzania waishio Marekani huko huko ilikotolewa
Tuzo?
Serikali
ya CCM imejenga Vyuo vya kutosha vinavyozalisha wasomi wa kutosha na
hata bomu tunalojiandaa kulikabili ni la vijana wasomi ambao hawana
ajira na sio vijana wasio na elimu kama anavyodai yeye.
IMETOLEWA NA TAWI LA CCM MAKAO MAKUU
DODOMA
28/05/2012