Monday, June 29, 2015
Nkupamah blog
Mtoto wa Rais Jakaya Kikwete anayesoma shule ya kimataifa ya Feza, Khalfan Jakaya Kikwete (17) ameiwakilisha vema Tanzania katika shindano la kusaka wanafunzi wenye akili nyingi 'Genius Olympiad' lililofanyika Oswego, Marekani mwaka huu.
Shindano
hilo huandaliwa na Idara ya Sayansi na Elimu ya Chuo Kikuu cha New York
likishirikisha shule za kimataifa duniani likihusisha kazi za masuala
ya sayansi, sanaa, biashara na mazingira.
Kwa
mujibu wa mtandao wa www.geniusolympiad.org, mwaka huu nchi 69
zilishiriki kwa kupeleka kazi 1,171. Kazi 401 zilikidhi vigezo na
kupokewa. Shule za kimataifa za Feza ziliwasilisha kazi nne na kushinda
medali moja ya dhahabu na tatu za shaba.
Kazi
iliyoshinda medali ya dhahabu iliitwa 'Vcardin' iliyoandaliwa na
kuwasilishwa na Khalfan na Seif Yahya Mhata ambao wote ni wanafunzi wa
shule za Feza.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki
iliyopita, Khalfan alisema kazi yao imelenga kurahisisha mawasiliano ya
kimataifa kwa kuwa na njia ya uhakika ya kuwasiliana.
"Mradi
huu unahusu kubadilishana kadi za mawasiliano kwa njia ya mtandao. Ni
muhimu sana kwa mawasiliano hasa ya wafanya biashara, lakini inahitaji
uwe na simu ya kisasa yenye intaneti au kifaa kingine chenye intaneti,"
alisema Khalfan aliyekuwa amefuatana na Mhata.
Kazi
nyingine kutoka Feza zilizoshinda medali za shaba ni 'The Fault of
Humanity' iliyoandaliwa na Prince Mwemezi ambaye alipiga picha ya moto
ukiunguza miti eneo la Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam na
kuonyesha athari za mazingira zitokanazo na uchomaji misitu.
Medali
nyingine ya shaba imeletwa katika shule ya Feza na wanafunzi wawili
Goodluck Komba na Sajjad El-Amin ambao walianza kazi inayoonyesha namna
mkaa unavyoweza kupatikana kupitia karatasi na takataka badala ya kukata
miti.
Veronica
Ndomba, mhitimu wa kidato cha sita mwaka huu katika shule ya Feza
Girls, aliandaa kazi ya kuzuia uchafuzi wa mazingira ya bahari kwa
kuelimisha watu kuhusu kutotupa taka, mafuta na uvuvi haramu baharini na
kushinda medali ya tatu ya shaba.
Nkupamah blog
0 comments :
Post a Comment