Tuesday, June 30, 2015
Nkupamah blog
SERIKALI imesema itawachukulia hatua kali wafanyabiashara wa mafuta, ikiwamo kuwafungia vituo vyao na pia kufuta leseni zao watakaobainika kugoma kuuza nishati hiyo.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage amewaonya wamiliki wa
vituo vya mafuta nchini wasije wakajiingiza katika mtego wa kufanya
mgomo wa kuuza mafuta katika vituo vyao.
Mwijage
alitoa tamko hilo wakati wa kipindi cha maswali na majibu ambapo Naibu
Spika, Job Ndugai alimtaka atoe tamko la Serikali kutokana na taarifa
zilizokuwa zikisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwamba wauza
mafuta wamepanga kugoma kuuza mafuta kuanzia leo ili kusubiri bei mpya
ya bidhaa hiyo.
Mwijage
alisema naye ameona taarifa hizo kwamba ndani ya siku mbili zijazo
kutakuwa na tatizo hilo la mafuta, lakini alilihakikishia Bunge kwamba
kuna hifadhi ya kutosha ya nishati hiyo na hakuna haja ya wananchi kuwa
na hofu.
“Nimeona
katika mitandao ya kijamii kwamba Taifa katika siku mbili zijazo
litakuwa na uhaba wa mafuta. Niseme hili haliwezi kutokea.
“Haliwezi
kutokea na haya si maneno ya kufurahisha. Haliwezi kutokea kwa sababu
tunajua kwa takwimu kwamba katika hifadhi za Dar es Salaam kuna mafuta
ya kutosha. Tunajua hilo.
“Haliwezi
kutokea kwa sababu sheria na kanuni zinampa mamlaka Waziri kuruhusu
mafuta yauzwe. Haiwezi kutokea kwa sababu sheria za Ewura zinaweza
kufungia mtu yeyote mwenye mafuta anayezuia mafuta kuuzwa,” alisema Naibu Waziri huyo.
Alisisitiza
kwa kuwaonya wenye mafuta nchini wasijiingize katika mtego huo kwa
kutaka kufanya uvumi huo utokee na kuwa kweli kwani hakuna sababu ya
kuzuia mafuta yasiuzwe.
Hata
hivyo, alisisitiza kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Boniface
Simbachawene pamoja na watendaji wengine wa wizara hiyo wanafuatilia
jambo hilo, ikiwa ni pamoja na kutafuta chanzo cha ujumbe huo.
Aliwataka
wenye mafuta kuruhusu yauzwe na watakaoenda kinyume basi vituo vyao
vinaweza kufungiwa na wale wenye hifadhi ya mafuta pia vitafungiwa na
leseni itachukuliwa kwa vile hiyo ni mali ya Waziri mwenye dhamana ya
masuala ya nishati na madini.
Juzi
mitandao mbalimbali ya jamii nchini ilikuwa na habari za kuwataka
wananchi kuweka mafuta kwa wingi kwenye magari yao kwa vile wenye mafuta
walikuwa wamepanga kugoma kuyauza kwa siku mbili zijazo, lengo ikiwa ni
kusubiri bei mpya kutoka Mamlaka ya Udhibiti ya Nishati na Gesi
(Ewura).
Nkupamahblog
0 comments :
Post a Comment