Sunday, June 28, 2015
Nkupamah blog
CHAMA
cha NCCR-Mageuzi kimesema hakitajitoa katika Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) pamoja na kuwapo kwa vikwazo vya ugawaji wa madaraka
ndani ya umoja huo.
Akizungumza
katika kikao cha Kamati Kuu cha chama hicho kilichoketi jana katika
Hoteli ya Travertine jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho,
James Mbatia, alisema lengo la umoja huo lilikuwa ni kuunganisha nguvu
ili kuwa na sauti moja ya ushirikiano.
“Yapo
maneno mengi yamesemwa na waandishi, wachochezi wanasema NCCR inataka
kuvunja Ukawa, tangu lini mama akakata mkono wa mtoto wake?
“Kama
kuna wenye wazo la sisi kujitoa kwenye umoja huu ni vizuri watambue
kuwa hatuna mpango huo, na hili ni azimio lililotolewa na wajumbe wa
Halmashauri Kuu. Pia itambulike kuwa chama hiki ni zao la Ukawa, hivyo
si jambo rahisi kujitoa,” alisema Mbatia.
Alisema Ukawa si sehemu ya kugawana madaraka na kudai kuwa umoja huo unaangalia zaidi masilahi ya wananchi.
Mbatia
alisisitiza pamoja na uchochezi uliopo na changamoto ya ugawaji
majimbo, wanaamini watavuka kwa kuwa lengo ni kusaidia wananchi na si
vyama husika.
Alisema
umoja huo umejipanga vizuri, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kwakuwa
wana uwezo wa kutoa rais pamoja na viongozi wengine watakaounda
Serikali.
Ajitosa Sakata la Zanzibar
Aidha
Mbatia alishagazwa na hatua ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
kuvunja Baraza la Wawakilishi juzi bila tukio hilo kuhudhuriwa na
Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad baada ya wabunge na
wawakilishi kumkatalia kuhudhuria.
“Nimeshangaa sana rais wa Zanzibar anavunja Bunge yupo mwenyewe bila Maalim Seif. Nini maana ya Serikali ya Umoja wa Kitafa?” alihoji Mbatia.
Alisema
wanachama wa vyama vya CCM na CUF wanapaswa kutambua kuwa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa ni makubaliano na mali ya Wazanzibari wote na si
wanasiasa pekee.
Akizungumzia
kuhusu mwenendo wa uandikishaji wa daftari la wapigakura unaosimamiwa
na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kutumia mfumo wa kielektroniki
(BVR), alisema hakuna dalili za daftari hilo kukamilika kwa wakati
kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji.
Alisema kutokana na hali hiyo, kuna viashiria vinavyoonyesha uchaguzi utakaofanyika Oktoba hautakuwa huru na wa haki.
“Uchaguzi
hautakuwa huru na haki kwa sababu wameshindwa uandikishaji, kama leo
wanasema kuna zaidi ya watu 5,000 wamejiandikisha mara mbili,
wanamaanisha nini kwa wananchi?
“Tulishauri
tangu mwaka jana kuhusu utaratibu wa uandikishaji na muda wa kuanza,
lakini wenzetu wakawa wanabisha. Kwa hapa tulipofikia lolote likitokea
wa kulaumiwa ni Serikali ya CCM,” alisema Mbatia.
Alisema
hadi sasa kuna baadhi ya mikoa ikiwamo Dar es Salaam na Pwani bado
hawajaandikishwa. Pia NEC inapaswa kuwa na muda wa kuhakiki majina
ambako kutafanywa na wananchi.
Aliongeza
kuwa Serikali ya awamu ya nne tangu ilipoingia madarakani mwaka 2005
imekuwa ikipoteza mvuto siku hadi siku kutokana na kutowajibika kwa
ufasaha.
Alisema
hadi sasa kuna mazingira ambayo mtu yeyote makini ni rahisi kuona jinsi
Serikali ya CCM ilivyopoteza utashi, mvuto na mwelekeo wa kuongoza
Watanzania.
Nkupamah blog
0 comments :
Post a Comment