Tuesday, June 30, 2015
Nkupamah blog
MKURUGENZI wa halmashauri ya wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Rustika Turuka amemweka mahabusu Ofisa Mtendaji Kata ya Kining’inila John Maduhu, kwa tuhuma za kutafuna Sh milioni 21 za ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari Kining’inila.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Turuka alisema
mtendaji huyo aligundulika kula fedha hizo baada ya mlezi wa kata hiyo
anayesimamia ujenzi wa maabara, Fedilis Mabula, kwenda katika kata hiyo
na kukuta jengo halijapauliwa huku halmashauri ikiwa imetoa fedha hizo
Sh milioni 21.
Alisema baada ya kufuatilia fedha hizo benki zilikuwa zimeshatolewa
kwa nyakati tofauti, jambo lililomfanya mkurugenzi huyo kumtafuta kwa
hali na mali mtendaji wa kata hiyo.
”Kwa kweli mtendaji huyo ameniudhi sana, mimi kama Mkurugenzi nilitoa
Sh milioni 21 za kupaua jengo la maabara katika sekondari ya
Kining’inila, lakini cha ajabu nimekwenda huko nimekuta jengo
halijapauliwa na nilipouliza uongozi wa kata hiyo walisema fedha
zimeliwa na mtendaji kata,” alisema.
Aidha mkurugenzi huyo alidai baada ya taarifa hiyo alilazimika kwenda
hadi Benki ya NMB tawi la Igunga ili kujua kama kweli mtendaji huyo
amezitoa fedha hizo benki.
Alipogundua fedha hizo zimetolewa alimtafuta mtendaji huyo ambaye
hata hivyo alimkwepa kwa muda wa zaidi ya wiki moja hadi juhudi
zilipofanyika ndipo alipokamatwa na kufikishwa kituo cha polisi huku
mtendaji huyo akiwa hana hata shilingi moja.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wilaya ya Igunga, Azizi Mayunga,
amethibitisha kukamatwa kwa mtendaji huyo Maduhu na kusema kuwa
upelelezi utakapokamilika anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya
kujibu tuhuma zinazomkabili.
Nkupamah blog
0 comments :
Post a Comment