Thursday, July 2, 2015
Nkupamah blog
Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara imezidi kupata pigo baada ya Mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji 16 vya mji mdogo wa Mirerani, kwa maelezo kuwa ulikiuka sheria na utaratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja
kwa Mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi huo ambao uliwaweka
madarakani makada wa CCM.
Awali, Mei 30 Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya
Kiteto ilitengua matokeo ya uchaguzi wa mwenyekiti wa Kijiji cha
Lobosireti kwa kukiuka sheria na utaratibu.
Chadema ilifungua kesi kadhaa mahakamani hapo
kupinga kitendo cha wagombea wa CCM kupewa ushindi bila kufanya uchaguzi
Desemba 14, mwaka jana.
Hukumu hiyo ya jana, inatokana na kesi
zilizofunguliwa na Chadema wilayani Simanjiro kwenye kata za Endiamtu na
Mirerani, wakipinga wagombea wa CCM kupewa ushindi bila kupigiwa kura
kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana.
Hakimu Mkazi Mfawidhi mahakama hiyo, Elimo Massawe
aliagiza kurudiwa kwa uchaguzi wa viongozi wa vitongoji vya Zaire,
Kisimani, Tenki la Maji, Endiamtu, Kairo na Kazamoyo vilivyoko Kata ya
Ediamtu.
Hakimu Massawe alitaja vitongoji vingine kuwa ni
Sekondari, Kilimahewa, Tanesco, Kazamoyo Juu, Mji mpya, Tupendane na
vitongoji vya Kata ya Mirerani ambavyo ni Kangaroo, Songambele A, Getini
na Songambele B.
Katika kesi hiyo, Chadema iliwakilishwa na
mawakili James Millya, Shadrack Kimomogoro na Daudi Haraka na Mahakama
iliamuru walipwe Sh160 milioni za gharama za kesi hiyo ambayo ilichukua
takribani miezi sita hadi kutolewa hukumu.
Katibu Mwenezi wa Chadema mkoani Manyara, Ambrose
Ndege alisema Mahakama imetenda haki kwa kutoa hukumu sahihi na
wanajipanga ipasavyo kuhakikisha watashinda vitongoji vyote pindi
uchaguzi huo utakaporudiwa.
“Tuliwaeleza tangu awali kuwa uchaguzi ukifanyika
tutawashinda saa nne asubuhi hivyo tunawasubiri uwanjani na tutaongoza
Mamlaka ya Mji wa Mirerani kwani wananchi wanatukubali,” alisema Ndege.
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa CCM wa Kata ya
Endiamtu, Mashaka Jeroro alisema wanatarajia kukata rufaa kupinga hukumu
hiyo akisema wagombea wa Chadema walikosea kujaza fomu ndiyo sababu
wakawekewa pingamizi.
Nkupamah blog
0 comments :
Post a Comment