Monday, July 13, 2015
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa maonyesho hayo ya Milan 2015 Bw. Bruno
Antonio Pasquino mara alipowasili.
Maalim Seif kwenye maonyesho ya kimataifa ya biashara Mjini Milan Italy. (Picha zote na Salmin Said, Italy)..
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akiwahutubia washiriki wa maonyesho hayo wakati wa kuadhimisho siku ya
Tanzania kwenye maonyesho hayo mjini Milan Italy.
Na: Khamis Haji, Milan Italy
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amefungua
milango kwa wafanyabiashra na wawekezaji wa Ulaya kutumia fursa nzuri za
uzalishaji wa biashara za viungo na utalii nchini ili kuweza kufungua
miradi yao.
Amesema
kwa miaka mingi Zanzibar imejulikana kama visiwa vya viungo (Spice
Islands) kutokana na utajiri mkubwa wa mazao hayo, hali ambayo
imechangia kukua kwa soko la utalii na kuimarisha uchumi wake.
Maalim
Seif amesema hayo alipokuwa akihutubia katika maadhimisho ya siku ya
Tanzania, kwenye maonyesho ya kibiashara ya kimataifa yanayofanyika
mjini Milan Italy, ambapo zaidi ya nchi 140 zinashiriki.
Amesema
sekta ya kilimo cha viungo kama karafuu na bidhaa nyengine
zinazozalishwa Zanzibar na Tanzania Bara, ni eneo linaloweza kupewa
kipaumbele na wafanyabiashara hao na kuweza kuwanufaisha wananchi wa
Tanzania ambao wengi wao ni wakulima.
Katika
sekta ya utalii Maalim Seif ambaye anamuwakilisha Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano kwenye maonyesho hayo amesema, vivutio vilivyopo
Tanzania ikiwemo Mji Mkongwe wa Zanzibar, Mlima Kilimanjaro, mbuga za
wanayama na fukwe, imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kipekee.
“Tanzania
tuna utajiri mkubwa wa rasilimali, tunayo gesi na mafuta, madini mbali
mbali ikiwemo Tanzanite, mazingira bora kwa kilimo na vivutio vya
utalii. Nakuombeni tumieni fursa hizi kuja kuwekeza”, amesema Maalim
Seif.
Ameishukuru
Serikali ya Italy kwa kuandaa maonyesho hayo na kuifanya Tanzania kuwa
miongoni mwa nchi washiriki, na kwamba kitendo hicho kinadhihirisha
uhusiano mwema uliopo kati ya Italii na Tanzania.
Mapema
akizungumza kwenye maonyesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa maonyesho hayo ya
Milan 2015 Bw. Bruno Antonio Pasquino ameelezea kuridhishwa na ushiriki
wa Tanzania kwenye maonyesho hayo, pamoja mazingira mazuri ya
uwekezaji.
Amesema
ushiriki huo ni fursa nzuri kwa Tanzania kuweza kujitangaza kwa mataifa
mbali mbali yanayoshiriki maonyesho hayo, ili hatimaye wawekezaji
waweze kuvutika na kuelekeza miradi yao nchini Tanzania.
Naye
Mkurugenzi wa banda la maonyesho la Tanzania bibi Twilumba Mlelwa
amesema bidhaa za kitanzania zilizopo kwenye maonyesho hayo zikiwemo za
viungo na sanaa, zimekuwa kivutio kikubwa kwa wageni.
Maalim
Seif pia alipata fursa ya kutembelea mabanda ya nchi mbali mbali kwenye
maonyesho hayo zikiwemo wenyeji Italia na Kazakstan ambayo inatarajiwa
kuandaa maonyesho kama hayo mwaka 2017, pamoja na kutembelea mabanda
yote ya nchi za Afrika Mashariki.
Maonyesho hayo yalipambwa kwa burudani maalum ya ngoma iliyochezwa na kikundi cha sanaa cha Bagamoyo.


0 comments :
Post a Comment