Kinara, Selemani Shabani Ulatule.
Makongoro Oging’ na Issa Mnaly, Mkuranga,GPL
WAKATI jeshi la polisi nchini likiendelea kuwasaka watuhumiwa wa mauaji
ya polisi na kupora silaha katika Kituo cha Stakishari, Ilala jijini
Dar, Uwazi limefanikiwa kuipata picha ambayo inadaiwa ni ya mtuhumiwa
kinara wa tukio hilo aliyetajwa kwa jina la Seleman Shaban Ulatule.
ENEO LA TUKIO
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wanahabari wetu walifika katika Kijiji cha
Mandikongo, Mkuranga, Pwani na wakazi wa maeneo ya jirani wakiwa katika
hofu baada ya watuhumiwa hao waliokuwa wakiishi jirani na kijiji hicho
kutoweka.
NGOME YAO YATEKETEZWA
Wanahabari wetu walioambatana na afisa mtendaji wa Kijiji cha
Mandikongo, polisi na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
walishuhudia makazi ya watu hao yakiwa yameteketezwa kwa moto na
wananchi wenye hasira kali.
WANANCHI WAZUNGUMZA
Wakizungumzia tukio hilo, wakazi wa kijiji hicho walisema majambazi hao
waliokuwa wamejitenga na makazi ya wanakijiji, walitoweka na familia zao
baada ya kupata taarifa kuwa kuna msako mkali unaofanywa na jeshi la
polisi ambao ulifanikiwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa, bunduki 15 za
kivita na fedha zaidi ya shilingi milioni 170.
WALIVYOFICHA FEDHA
Wakizidi kuelezea tukio hilo, wakazi hao waliwaonesha waandishi wetu
shimo ambalo walilitumia kuhifadhia fedha hizo ambapo juu yake waliweka
kinyesi cha binadamu kilichokadiriwa kuwa ni cha watu saba ikiwa ni
alama yao ambayo pia itamfanya mtu akisogelea eneo hilo alipitie mbali
kwa kuona kinyaa.
“Tunaomba vyombo vya usalama kuhakikisha watuhumiwa wote wanapatikana na
silaha nzito walizokimbia nazo maana wanaweza kuja kukivamia kijiji
hiki na kufanya unyama wa kutisha pindi vikosi vya usalama
vitakapoondoka hapa,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyeomba
hifadhi ya jina lake gazetini.
MTENDAJI AZUNGUMZA
Afisa mtendaji wa kijiji hicho, Issa Said Mchalaganga aliwataja
watuhumiwa ambao walikuwa wakiongozwa na kinara wao Seleman Shaban
Ulatule ni pamoja na Said Mohamed Ulatule, Ally Mohamed Ulatule, Hamis
Mohamed Ulatule, Haji Seleman Ulatule na Ally Said Ulatule.
“Hao wote walikimbia nyumba zao na baadaye kuharibiwa na wananchi kwa kuteketezwa kwa moto,” alisema Mchalaganga.
WALIOKAMATWA
“Katika msako wa vyombo vya usalama walifanikiwa kumkamata Ramadhani
Hamis Ulatule na mwenyekiti wa kijiji, Ramadhani Mohamed Ulatule kwa
ajili ya mahojiano na kwa kweli tunampongeza Kamishna Suleiman Kova na
vyombo vya usalama kwa kazi nzuri ya kubaini kikundi hiki na kufanikiwa
kupata baadhi ya silaha,” alisema mtendaji huyo.
MAISHA YAO KIJIJINI HAPO
Wananchi wa kijiji hicho waliliambia Uwazi kuwa, watu hao ambao
wanadaiwa kuwa majambazi kabla ya kubainika, walikuwa wakiishi maisha ya
usiri na wakifanya mafunzo ya kijeshi porini.
WALIJITENGA NA SERIKALI
“Hawakupenda kushiriki na wanakijiji katika shughuli za maendeleo,
upigaji kura, uhesabuji wa watu hata hospitali ya hapa walikuwa hawaji
kupata huduma na haikujulikana walikokuwa wakipatia matibabu,” alisema
mwanakijiji mmoja.
YADAIWA KUNA ASKARI ALIYEKUWA AKIWATEMBELEA
Wananchi wa kijiji hicho walidai kuwa, kulikuwa na askari mmoja wa
Gereza la Dondwe lililopo karibu na kijiji hicho ambaye alikuwa rafiki
wa majambazi hao aliyekuwa akiwatembelea mara kwa mara katika makazi
yao.
“Huyo askari tulikuwa tunamuona akienda huko porini mara kwa mara sasa
tangu tukio litokee hajaonekana, tunaiomba serikali imfuatilie,” alisema
mkazi mwingine wa kijiji hicho.
WALIKATAA KUHESABIWA
Afisa mtendaji wa kijiji hicho aliwaeleza waandishi wetu kuwa walimtilia
shaka kiongozi wa ukoo wa Ulatule, Seleman Shaban ambaye aliwahi
kuandikiwa barua na mkuu wa Wilaya ya Mkuranga yenye kumbukumbu namba
AB/226/290/1/40 ya Agosti 31, mwaka 2012 (nakala tunayo) ikimhoji kwa
nini aliwakataza watu wa eneo lake kuhesabiwa kwenye sensa.
“Hapo ndipo tulipotilia shaka haswa baada ya tukio hili kutokea. Seleman
alikuwa hataki kabisa kujihusisha na shughuli za serikali. Hata wakati
wa zoezi la sensa aliwakataza watu wa eneo lake kuhesabiwa,” alisema
mtendaji huyo.
WALIISHI NA RAIA WA KIGENI
Uchunguzi unaonesha kwamba watu hao hawakupenda wananchi kutembelea wala
kukatisha katika makazi yao na kulikuwa na nyumba nyingine jirani
ambazo zinadaiwa walikuwa wakiishi watu wasio Watanzania.
SABABU YA KUVAMIA VITUO VYA POLISI NI NINI?
Inadaiwa kuwa kuna majambazi wana mpango wa kuanzisha kikosi kikubwa
kama jeshi la kupambana na dola ambayo imewashikilia wafuasi wao katika
magereza mbalimbali nchini.
Imeelezwa kwamba, utaratibu huo ulikwepo tangu zamani na walikuwa
wakipata silaha za kivita kutoka kwa wakimbizi wa nchi jirani lakini
hali hiyo ikadhibitiwa na serikali kukawa hakuna silaha inayoingia
nchini kinyume na taratibu.
WABADILI MBINU
Inasemekana kwamba baada ya kuwa na uhaba wa silaha wakawa wanawavamia
polisi katika vituo, mabenki na popote pale wanapofanyia doria wakiwa na
silaha kisha kuwapora.
Uchunguzi mwingine unaonesha kwamba walioua katika Kituo cha Polisi
Stakishari ni baadhi ya kikosi chao na baada ya kufanya mauaji walipitia
Barabara ya Nyerere na kuingia Banana kuelekea Kitunda, Msongola,
Mbande kisha kuingia katika pori la Kijiji cha Mandikongo.
Kamishna Kova alipoulizwa kuhusu mzee Ulatule na sakata zima la kambi
hiyo ya watu hao waliotoroka alisema, suala hilo atalizungumzia Ijumaa
kwa sababu ndiyo siku aliyopanga kuzungumza na waandishi wa habari.
“Siku hiyo ndiyo niliyopanga kuzungumza na waandishi wa habari hivyo uje na swali hilo nitalijibu,” alisema.
TUJIKUMBUSHE
Julai 12, mwaka huu watu wanaokadiriwa 16 walifanya uvamizi katika Kituo
cha Polisi Stakishari na kuua polisi wanne na raia watatu kisha kupora
silaha zaidi ya 24 ambapo Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es
Salaam, Kamishna Suleiman Kova na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi
Ilala, SACP Lucas Mkondya waliapa kuwakamata watuhumiwa hao na silaha
walizoiba.
Msako wa polisi katika ngome hiyo iliyokuwa jirani na Kijiji cha
Mandikongo, polisi walifanikiwa kupata bunduki 15 ambazo baadhi ni zile
zilizoporwa katika Kituo cha Stakishari.


0 comments :
Post a Comment