Katibu wa Taasisi ya Zanzibar
Heart Foundation Sururu Abass Othman akizungumza na wananchi wa shehia
za Muembemakumbi, Karakana na Chimbuni waliofika kuchungaza Afya zao.
Picha na Makame Mshenga Maelezo Zanzibar
Mratibu wa Muungano wa Taasisi
zinazoshughulikia maradhi yasiyoambukiza Zanzibar (ZNCDA) Omar Abdalla
Ali akiwaelimisha wananchi waliofika kituo cha Afya Karakana kuchunguza
afya juu ya maradha ya maradhi hayo na njia bora za kujikinga.
Muuguzi wa Kituo cha Afya Karakana
Mere Hamad Jadi akiwapima wananchi maradhi ya sindikizo la damu
wakati wa zoezi hilo lililofanyika Kituo cha Afya cha Karakana nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar.
…………………………………………………………….
Na RAMADHANI ALI/MAELEZO ZANZIBAR.
Muungano wa Taasisi
zinazoshughulikia maradhi yasiyoambukiza Zanzibar (ZNCDA) umeishauri
Serikali na Mashirika wahisani kuelekeza nguvu zao katika mapambano
dhidi ya maradhi hayo kwa vile hivi sasa yamekuwa tishio kwa maisha ya
wananchi kuliko maradhi mengine yoyote Zanzibar.
Mratibu wa ZNCDA Omar Abdalla Ali
alitoa ushauri huo wakati wa zoezi la kuwapima afya wananchi wa
shehia za Karakana, Chimbuni na Muembemakumbi, Mkoa Mjini Magharibi
Unguja, lililofanyika Kituo cha Afya cha Karakana.
Alisema maradhi ya Sindikizo la
damu, Kisukari na Saratani yamejitokeza kuwa tishio kwa wananchi
kutokana na uelewa wao mdogo juu ya maradhi hayo na wengi kutokuwa na
mwamko wa kupima afya zao.
Alizitaja sababu zinazochangia
kuongezeka maradhi yasiyoambukiza kuwa ni mabadiliko ya mfumo wa
maisha ambao wananchi hupenda zaidi starehe kuliko kujituma, uvutaji
sigara, ulevi wa kupindukia na kutumia chakula cha makopo kilichotiwa
kemikali.
Akitowa takwimu ya maradhi hayo,
Omar alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2011 asilimia 33
ya wananchi wa Zanzibar wanakabili na sindikizo la damu na asilimia
nne wanamaradhi ya kisukari na taarifa kutoka Hospitali ya Ocean Road
Dar es Salaam zinasema kuwa kila mwaka wanapokea kiasi cha wagonjwa
1000 wa magonjwa ya saratani kutoka Zanzibar.
Aliongeza kuwa saratani ya matiti
na shingo ya kizazi kwa akinamama na tenzi dume kwa wanaume
zinaongoza kati ya wagonjwa wanaopelekwa huko kupatiwa matibabu.
Alisema taarifa hizo zinatisha
kutokana na idadi ndogo ya wananchi wa Zanzibar na ni sababu
iliyopelekea ZNCDA kufanya juhudi ya kutoa taaluma kwa wananchi,
kuwapima afya ndani ya shehia zao na kuwapa ushauri unaofaa wa kujikinga
na maradhi hayo.
Aliwataka wananchi kuanzisha
utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kujua afya zao mapema
badala ya kusubiri kuathiriwa na maradhi ndipo wakimbilie Hospitali.
“Maradhi yanapogundulika mapema ni
rahisi kuyatibu lakini unaposubiri mpaka yakakuathiri inakuwa vigumu
kuyatibu pimeni afya zenu kila wakati, ” alisisitiza Mratibu wa ZNCDA.
Aliwashauri viongozi wa Serikali
za mitaa, wabunge ,wawakilishi na madiwani, kuwasaidia wananchi kwa
kuwawekea vifaa vya kupima afya zao katika sehemu wanamoishi kwa vile
vifaa hivyo havina gharama kubwa.
Jumla ya wananchi 174 kutoka
shehia hizo tatu walipata nafasi ya kuangaliwa afya zao na maradhi ya
sindikizo la damu yamegundulika kuongoza katika shehia hizo.
0 comments :
Post a Comment