Wanachi wakitaharuki vyombo vilivyoweka juu ya kaburi marehemu, Jesca Onesmo.
Wahenga
walisema ukisitajabu ya Musa utaona ya Farao, hivi ndivyo ilivyokuwa
kwa wananchi wa mji wa Bariadi mkoani Shinyanga waliofurika katika
kaburi la marehemu, Jesca Onesmo (28), ambaye alifariki kisha kuwekewa
samani na vyombo vyake mbalimbali juu ya kaburi lake.
Marehemu, Jesca Onesmo enzi za uhai wake.
Ilikuwa
asubuhi ya saa mbili, Julai 7, mwaka huu ambapo baadhi ya wananchi wa
Mtaa wa Marambo, Bariadi waliokuwa wamepata msiba walipokwenda eneo la
Makaburi ya Kidinda kwa ajili ya kutafuta mahali pa kuchimba kaburi,
walipofika eneo hilo walipigwa na butwaa baada ya kuona kaburi moja
likiwa limewekewa vitu juu, hali ambayo ilitafsiriwa kuwa amezikwa
navyo.
Uwazi
baada ya kupewa habari hiyo lilifika katika eneo hilo na kukuta samani
za ndani, godoro na vyombo mbalimbali vikiwa vimerundikwa juu ya kaburi
hilo na baada ya uchunguzi ikajulikana kuwa ni kaburi la Jesca.
Mwananchi
mmoja ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema: “Kwa kweli
hili ( la kurundikwa vyombo vyake juu ya kaburi) limetushangaza sana na
ni la kwanza kutokea hapa Bariadi, hata sisi hatujui sababu lakini
labda ni ushirikina.”
Baada
ya tukio hilo polisi waliarifiwa ambapo walifika makaburini na kuamua
kuvipakia vyombo hivyo kwenye gari la polisi na kuvipeleka kituoni na
baada ya kufika huko walivifanyia upekuzi na kugundua vitu mbalimbali.
Habari
za kipolisi zinasema walikuta pochi ya marehemu ambayo ndani yake
ilikuwa na shilingi 13,000 pamoja na simu ndogo lakini pia walifanikiwa
kukuta cheti cha hospitali kilichoonesha marehemu alikuwa mgonjwa na
alikuwa anatumia dawa kila siku.
Aidha,
walipata pia daftari la mchango wa kifo ambalo lilionesha kuwa
alichangiwa na walipata jina na namba za simu ya dada yake (jina
linahifadhiwa) ambaye inadaiwa kuwa ndiye aliyehusika kumzika ingawa
baada ya kumpigia simu hakupokea na walipomfuatilia walikuta ametoroka
na familia yake, hadi sasa haijafahamika alipo.
Hata
hivyo, baada ya tukio hilo kutangazwa na vyombo vya habari baadhi ya
wananchi walidai kuwa marehemu alikuwa anaishi na mume wake huko
wilayani Kahama na hawakujua nini kilitokea hadi kuzikwa na kurundikiwa
vyombo juu ya kaburi lake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Gemini Mushy amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo.
“Tukio
hilo lipo lakini tunaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo chake
na sababu ya kumzika na vyombo vyake,” alisema kamanda huyo.


0 comments :
Post a Comment