Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Jitihada za
muongo mzima wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete kuimarisha na kudumisha Utawala Bora katika
Tanzania zimetambuliwa kimataifa kwa Rais kutunukiwa Tuzo la Utawala
Bora Barani Afrika mwaka 2015 (Good Governance in Africa.)
Rais Kikwete ametunukiwa Tuzo hiyo na Taasisi ya African Achievers Awards
yenye makao yake makuu katika Afrika Kusini kutokana na kutambua
mchango wake mkubwa katika kulea, kuimarisha, kuendeleza na kudumisha
Utawala Bora katika Tanzania katika miaka yote 10 ya uongozi.
Rais
Kikwete anajiunga na watu wachache ambao wamepata kupokea tuzo hiyo
tokea lilipotolewa kwa mara ya kwanza kwa Askofu Mkuu Desmond Tutu wa
Afrika Kusini mwaka 2011 kwa kutambua mapambano yake katika kutetea haki
za binadamu,usawa, haki na amani.
Rais Kikwete ameteuliwa kutoka miongoni mwa zaidi ya watu 1,202 ambao
majina yao yaliwasilishwa kwenye Jopo la Kimataifa Linalojitegemea na
lenye wajumbe kutoka Uingereza na Afrika Kusini kwa ajili ya uteuzi.
Kutokana na
tunuku hiyo, Rais Kikwete amealikwa kwenda Afrika Kusini kupokea tuzo
hiyo katika sherehe kubwa inayofanyika jioni ya kesho, Jumamosi, Julai
25, 2015 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Sandton (Sandton
Convention Centre) mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Kwa sababu
ya kukabiliwa na shughuli nyingi hapa nyumbani, Rais Kikwete amemwomba
Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Asha Rose Migiro, kumwakilisha
katika sherehe ya kupokea tuzo hiyo ambako pia atatoa mada kuhusu “Umoja wa Afrika: Fursa na Changamoto (Africa’s Unity: Prospects and Challenges) “ kwa niaba ya Rais Kikwete.
Tuzo za African Archievers Awards
zinalenga kuwatambua watu binafsi na taasisi ambazo zimejitambulisha
kwa michango yao kwa ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika.
Katika barua ya kumjulisha Rais Kikwete kuhusu uteuzi wake, Mtendaji wa African Achievers Awards, Bwana Rex Indaminabo amesema:
“Uongozi wa African Achievers Awards unayo furaha kukujulisha juu ya
uteuzi wako wa kupokea Tuzo la 2015 African Achievers Awards katika
kundi la Utawala Bora Barani Afrika.”
Ameongeza Mtendaji huyo: “Ni
kwa furaha na heshima kubwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri na Taasisi
ya Uongozi na Menejimenti wanakuandikia kukupongeza kwa kuteuliwa
kwenye orodha ya mwisho na hatimaye kuwa mshindi wa Tuzo la African
Achievers Awards katika kundi la Utawala Bora katika Afrika.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
24 Julai, 2015
0 comments :
Post a Comment