Mwenyekiti wa Bodi ya REA
Edmund Mkwawa, akiongea jambo wakati wa kikao kazi baina ya REA, taasisi
za Kifedha, Washirika wa Maendeleo na Taasisi Binafsi, Wizara , Taasisi
za Serikali, kilicholenga kujadili na kuangalia namna sekta hizo
zinavyoweza kushirikiana pamoja na kuongeza nguvu ili kuongeza kasi ya
kuviunganisha vijiji na umeme
……………………………………………………………………..
Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Taasisi za Kifedha, Taasisi
Binafsi na Washirika wa Maendeleo nchini, wameshauriwa kuona fursa
zilizopo katika sekta ya nishati hususani umeme kushirikiana na
serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ili kuwezesha
mapinduzi ya maendeleo na kuhakikisha kwamba vijiji vingi zaidi
vinaunganishwa na nishati ya umeme.
Hayo yamebainishwa nyakati
tofauti katika kikao kazi kilichoandaliwa na REA, kikijumuisha Taasisi
za Kifedha, Taasisi Binafsi, Washirika wa Maendeleo Washirika katika
tasnia ya nishati, wawakilishi kutoka Wizara na Taasisi za Serikali, kwa
lengo la kujadili na kuangalia namna sekta hizo zinavyoweza
kushirikiana pamoja na kuongeza nguvu ili kuhakikisha kwamba Tanzania
hususan vijiji vinaunganishwa na nishati ya umeme ikiwemo kuchochea
shughuli za kiuchumi vijijini kupitia nishati hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho,
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava
amesema miradi ya kuviunganisha vijiji na nishati ya umeme ni eneo
linalohitaji kuendelezwa kwa ushirikiano na wadau hao ili kuongeza kasi
ya uunganishaji umeme.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya REA
Edmund Mkwawa, ameeleza kuwa, endapo wadau hao watashirikiana na REA,
mradi huo utaleta matokeo makubwa zaidi ya yaliyopatikana sasa na hivyo
kuweza kuyafikia maeneo ambayo hayajafikiwa na nishati hiyo. Aliongeza
kuwa, zipo fursa nyingi ambazo taasisi hizo zinaweza kuzitumia kupitia
miradi mbalimbali ambayo itaziwesha kupata faida.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Nishati Vijini (REA), Dr. Lutengano Mwakahesya alitumia fursa
hiyo kuwashukuru wadau wote ambao wamewezesha Wakala huo kuunganisha
miji na vijiji na nishati hiyo na kufikia asilimia 40 na kueleza kuwa,
Wakala huo utaendelea kutafuta wafadhili ili kuweza kufanikisha malengo
yake ya kuhakikisha kwamba taifa linaunganishwa na umeme.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi
anayeshughulikia nishati kutoka Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB),
Stella Mandago, amezitaka taasisi hizo kufanya kazi na Wakala huo kwani
zipo fursa nyingi na hivyo itawezesha taasisi hizo kupanua wigo wa
shughuli zao kupitia nishati ya umeme.


0 comments :
Post a Comment