Polisi wakiimarisha ulinzi karibu na nyumbani kwa mgombea urais
kupitia CCM, Dk John Magufuli chato mkoani Geita baada ya kutangazwa
kugombea nafasi hiyo mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho,
mjini Dodoma jana. Picha na Baraka Rwesiga
Muda mfupi baada ya kuwapo taarifa kuwa Magufuli anaongoza kura za
wajumbe wa Mkutano Mkuu, aliongezewa ulinzi usiku huo na hadi jana muda
wote, alionekana akiwa na walinzi watano.
Jimboni Chato, nyumbani kwake eneo la Rubambambangwe, polisi walionekana wakitanda tangu jana asubuhi tofauti na siku nyingine.
Askari hao wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, Alex Mkama
walionekana nyumbani hapo tangu asubuhi hata kabla matokeo yaliyompa
ushindi Dk Magufuli hayajatangazwa.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikwenda nyumbani kwa Dk Magufuli
kuzungumza familia yake, hakuruhusiwa na polisi waliokuwa kwenye lango
kuu la kuingilia, walidai wamepewa maelekezo ya kutoruhusu watu kuingia.
“Naomba usiingie ndani wala kupiga picha eneo hili, hayo ndiyo maelekezo
ninayokupa na niliyopewa, vinginevyo mtafute RPC (Kamanda wa Polisi
Mkoa) akupe ruhusa,” alisema mmoja wa askari hao. Akizungumzia hali
hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema polisi
walikuwa wanatekeleza jukumu lao kwa umma la kulinda raia na mali zao
kutokana na wananchi kwa makundi kusherehekea ushindi wa mteule huyo.
Konyo alisema ulinzi huo ulilenga kuweka na kuimarisha usalama kwenye makazi ya familia hiyo.
Hata hivyo, Konyo alipotakiwa kuzungumzia kuzuia watu kupiga picha
kwenye makazi hayo alikata simu na hata alipopigiwa tena hakupokea.
Nyumbani kwake, Ada Estate, ulinzi ulianza kuimarishwa mara tu baada ya
kiongozi huyo kutangazwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM.
Mmoja wa walinzi hao ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema
wameongezwa walinzi wengine wanne mara baada ya matokeo ya mjini Dodoma
kutangazwa.
Magari kadhaa yenye namba za serikali na magari ya polisi yalionekana yakiingia na kutoka nyumbani kwa Magufuli.
Kadhalika kama ilivyokuwa Chato, walinzi hao walisema wamepewa amri
kutoruhusu watoto au mwanafamilia yeyote kutoka nje au kuzungumza na
waandishi wa habari.
Majirani wanena
Baadhi ya majirani walimtaja mke wa Magufuli, Janeth Magufuli kuwa ni
mtu asiye na makuu na anayechangamana na wengine katika masuala ya
kijamii.
Mmoja wa majirani hao, aliyejitambulisha kwa jina la Yahya alisema
Janeth ni jirani mnyenyekevu na mkimya ambaye anashiriki mambo mengi ya
kijamii katika eneo hilo la Ada Estate.
“Ukikutana naye hutajua kama ni mke wa waziri, mkimya, wakati mwingine
anaenda zake mazoezi, anasali jumuiya na wala hana neno na mtu,”
alisema.
Jirani mwingine, Josephina Murungu alikuwa na maoni tofauti juu ya
familia ya Magufuli akisema kutokana na hadhi yao, ni vigumu kuwaomba
kiberiti au chumvi.
“Siku zote watu matajiri huwezi hata kuwaomba chumvi, wala kibiriti,
ndiyo maana tunashindwa kuwa nao karibu, si kama majirani wengine, kwa
kifupi tunawaogopa,” alisema.
Jirani mwingine Sayuni Msungwa, anayesali nao kwenye Jumuiya na Janeth,
alisema wamezoea kukutana kwenye maombi na anamwona ni mwanamke asiye
na makeke wala kupenda kujikweza.
“Ukikutana naye kwenye jumuiya anaonekana mpole sana, huwa namsalimia na
ananijibu kwa unyenyekevu, siyo wa kuvaa mavazi ya gharama au vidani,
walaaa… mpole tu,” alisema.
Chato wamzungumzia
Baadhi ya wakazi wa mjini Chato, walisema Mkutano Mkuu wa CCM umetenda haki na Dk Magufuli ndiyo chaguo la Watanzania.
Kada wa CCM, Steven Kasika alisema ana imani kubwa na Dk Magufuli hivyo
kuchaguliwa kwake si tu kwamba atawarejeshea matumaini wananchi na
wanachama wa chama hicho, bali pia wapinzani watamuunga mkono kwa sababu
anao uwezo wa kuongoza nchi.
George Mpanduji ambaye ni Katibu wa Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania
(Tacoga), alisema kuchaguliwa kwa Dk Magufuli kutaisaidia CCM kushinda
na kuinusuru sekta ya kilimo.
Mkurugenzi wa Shule ya Emmau English Medium mjini Chato, Onesmos Nyaruba
alisema matumaini yake kwa mteule huyo ni makubwa hasa kurejesha imani
ya wananchi kwa CCM, ambayo walikuwa wameipoteza.
“Magufuli ni mwajibikaji hivyo mwisho wa mafisadi umefika,
atawawajibisha wote waliojilimbikizia mali kinyume na misingi ya chama
chake,” alisema Nyaruba.
MWANANCHI


0 comments :
Post a Comment