Taharuki yaibuka machimbo ya Nyangalata, waliofukiwa wadaiwa kuwa hai

Kahama. Wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Nyangalata wilayani Kahama, wameingiwa na hofu baada ya uvumi kwamba wenzao sita kati ya saba waliofukiwa na kifusi siku 42 zilizopita bado wapo hai.

Hali hiyo ya hofu iliibua upya tukio hilo na kusababisha waokoaji na watoa huduma kutoka kikosi cha uokoaji kuanza kazi ya kufukua shimo walimofukiwa wachimbaji hao, wakiwa na imani kwamba ni wazima.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyangalata, Abdul Komba alisema hali hiyo iliibuka baada ya wachimbaji kwenye mashimo jirani na shimo husika walipodai kuwa watu hao wapo hai na kwamba, walipokuwa shimoni walisikia wakizungumza.

“Mpaka sasa watu wapo wengi sana wakijaribu kufukua kupitia mashimo jirani na kila anayeingia chini anarudi na kudai amewasikia wakiongea na kuwa walipojaribu kuwasemesha waliwajibu,” alisema Komba.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa alisema anafuatilia suala hilo ili kujua ukweli wake, ingawa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema halina ukweli licha ya kutaka ufuatiliaji zaidi ufanyike.

Mwanzoni mwa Oktoba, mwaka huu mashimo katika mgodi huo yalititia na kusababisha vifo vya watu saba ambao walikuwa wameingia ndani kwa lengo la kuwaokoa wenzao waliokuwa wamefunikwa na kifusi.

Baada ya kuwaokoa wenzao, wachimbaji hao walipatwa na mkasa huo kutokana na kukatika kwa kifusi kingine kilichowafunika hadi leo.

Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mgodi wa Shigomico, Hamza Tandiko alisema kwa mujibu wa wataalamu wa uokoaji kutoka mgodi wa Bulyanhulu, wachimbaji hao walifukiwa umbali wa mita 100.

Tandiko alisema kuwafukua kulihitaji gharama kubwa, lakini baada ya tukio la juzi la kudaiwa wapo hai, waokoaji wameanza upya ufukuaji kwa njia za kienyeji kuwatafuta chini ya mashimo hayo.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga alipotembelea eneo hilo alisema kuwatoa watu hao ardhini ni kazi ngumu inayohitaji mitambo mikubwa yenye uwezo wa kufukua eneo lote la mgodi ili kuwafikia.

Alisema kutokana na changamoto iliyopo, kazi hiyo ingehitaji muda mrefu na wataalamu zaidi.

MWANANCHI
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment