Wataalamu wa Gesi wametakiwa kujifunza kwa Mkandarasi

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kulia) akimsikiliza Meneja wa Kampuni ya GASCO, Mhandisi Mhandisi Kapuulya Musomba (katikati). Wa Kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Paul Masanja.
Kituo cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba
Baadhi ya mitambo kwenye Kituo cha kuchakata Gesi Asilia cha Madimba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kushoto) na Naibu wake, Mhandisi Paul Masanja mara baada ya kukagua Kituo cha Kuchakata Gesi asilia cha Madimba.

Wataalamu wa Kitanzania wanaofanya kazi kweye Mradi Mkubwa wa Gesi Asilia nchini wametakiwa kuhakikisha wanajifunza kwa ukamilifu shughuli zote za mradi huo kabla mkandarasi hajaondoka.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Omar Chambo na Naibu wake, Mhandisi Paul Masanja walipofanya ziara kwenye mradi huo kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa mradi huo.

Mbali na hilo, wafanyakazi hao walielezwa umuhimu wa kutanguliza uzalendo mbele katika shughuli zao ili kuleta tija.

Mhandisi Chambo aliwataka wafanyakazi hao kutobweteka na badala yake wawe makini kujifunza masuala yote yanayohusu mradi huo ili pale mkandarasi anapomaliza muda wake waweze kueendesha wao wenyewe bila kukwama.

“Itafika wakati lazima Mkandarasi ataondoka hivyo kama mtashindwa kujifunza kipindi hiki itawapa shida siku za usoni, kwahiyo hakikisheni mnajifunza kila anachokifanya,” aliagiza Mhandisi Chambo.

Kwa upande wake Mhandisi Masanja aliwataka viongozi wa mradi huo kuandaa utaratibu wa kuweka wazi kazi zinazofanywa na mkandarasi ili kila mfanyakazi aelewe nini kinafanyika bila kuwepo na kizuizi cha aina yoyote.

“Kusiwepo na kizuizi chochote cha nyinyi kuelewa shughuli zinazofanywa na Mkandarasi. Pale ambapo mnafikiri bado vijana hawajaiva vizuri hakikisheni mkandarasi anawaelekeza.

Vilevile aliwaagiza kuboresha mazingira ya kazi na pia kuandaa utaratibu utakaovutia vijana hao wa Kitanzania kuendelea kulitumikia Taifa lao kupitia mradi huo wa Kitaifa.

“Mtazame namna ambayo itawavutia wataalamu wetu waendelee kufanya kazi bila kufikiria kuondoka; mnaweza wapa mafunzo hao ukashangaa wanahama na hivyo kusababisha kudorora kwa baadhi ya shughuli,” alisema.
Naye Meneja wa Kampuni ya Gesi Asilia (GASCO), Mhandisi Kapuulya Musomba alieleza utaratibu unaotumiwa na wafanyakazi hao katika kujifunza shughuli mbalimbali za mradi.

Alisema wanaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na mkandarasi kwa lengo la kuelewa shughuli zinazofanyika ikiwa ni pamoja na matengenezo na uendeshaji wa mitambo.

“Tupo nao kwa ukaribu sana; wanatueleza nini watatufundisha na kwa muda gani. Tunawauliza maswali, tunatazama namna wanavyoendesha shughuli za hapa; hivyo nina imani muda wao wa kuondoka ukifika vijana wetu watakuwa wameiva vya kutosha kuweza kusimamia mradi huu,” alisema.

Lengo kuu la ziara hiyo ilielezwa kuwa ni kujionea shughuli zinazoendelea kwenye mradi huo mkubwa wa Kitaifa wa gesi asilia pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa mradi huo.

Maeneo ambayo yalitembelewa na viongozi hao ni pamoja na Kituo cha Kupokelea Gesi Asilia ya Mtwara na Lindi cha Somangafungu (Somangafungu Gas Receiving Station) kilichopo wilayani Kilwa, mkoa wa Lindi; Visima vya Gesi Asilia vya Mnazi Bay na Msimbati; Sehemu iliyoathiriwa na Mmomonyoko wa ardhi ya Msimbati na Kituo cha Kuchakata gesi asilia cha Madimba cha mkoani Mtwara.

Wengine walioongozana na viongozi hao katika ziara hiyo ni Kamishna wa Nishati, Mhandisi Hosea Mbise, Kamishna Msaidizi wa Nishati sehemu ya Gesi Asilia, Mhandisi Norbert Kahyoza, Meneja wa Kampuni ya Gesi Asilia (GASCO), Mhandisi Kapuulya Musomba na Maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa viongozi wao tangu wameteuliwa na huku ilielezwa kwamba ni miongoni mwa mikakati waliojiwekea ya kutembelea na kukagua miradi iliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake na vilevile kuzungumza na wafanyakazi wa miradi hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment