Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la
Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bwana Bonaventure Baya (aliyesimama),
akizungumza wakati wa kumkaribisha kwa mara ya kwanza Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Luhaga
Mpina (aliyekaa mbele) wakati alipofanya Ziara yake katika Makao Makuu
ya Ofisi hiyo kwa ajili ya kujitambulisha na kuangalia utendaji wa
Baraza hilo. (Picha na OMR)
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Luhaga Mpina
(aliyekaa mbele), akizungumza na baadhi ya watendaji wa Baraza la
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wakati alipotembelea kwa mara ya kwanza
Makao Makuu ya Ofisi ya Baraza hilo jijini Dar es Salaam leo. (Picha na
OMR)
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Luhaga Mpina (aliyekaa
katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Wafanyakazi wa
Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wakati alipofanya Ziara yake ya
kwanza kwenye Makao Makuu ya Ofisi hizo jijini Dar es Salaam leo. (Picha
na OMR)
…………………………………………………………………………..
Na Victor Mariki – Ofisi ya Makamu wa Rais
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu Rais – Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Luhaga Mpina amefanya
ziara yake ya kwanza tangu kuteuliwa kwake wadhifa wa unaibu waziri
kwa kutembelea Makao Makuu ya Baraza la Usimamizi wa Mazingira
(NEMC).
Katika ziara hiyo ya kujitambulisha pamoja na kukagua utendaji wa
Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mheshimiwa Mpina alibaini
baadhi ya changamoto zinazolikabili Baraza hilo katika utekelezaji wa
majukumu yake ikiwa pamoja na kuzipatia utatuzi changamoto hizo.
Aliongeza kwa kuainisha changamoto hizo kuwa ni; uchelewaji wa
utoaji vyeti vya Tathimini ya Athari kwa Mazingira kwa wateja,
utozaji tozo usioendana na wakati, uchache wa kanda na uchache wa
rasimali watu katika utekelezaji wa majukumu.
Aidha katika kutatua changamoto hizo Mheshimiwa Mpina alilitaka Baraza
hilo kuwasilisha viwango vya utozaji tozo vilivyowekwa kulingana na
Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 katika Ofisi ya Waziri ili viweze
kujadiliwa pamoja na wadau na kufanyiwa maboresho kulingana na wakati
huu.
Pia alilitaka Baraza hilo kutoa vyeti vya Tathimini ya Athari kwa
Mazingira kwa wateja wake ndani ya siku 60 kulingana na Sheria hiyo ya
Mazingira ya Mwaka 2004 ikiwa ni pamoja na kuviwasilisha vyeti hivyo
katika Ofisi ya Waziri ili viweze kutolewa na Ofisi ya Waziri ndani ya
siku 30.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Mpina alitoa agizo la siku 30 tu kwa Baraza
la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kukamilisha utoaji wa vyeti 512
vilivyocheleweshwa utolewaji wake na Baraza hilo kulingana na Sheria ya
Mazingira ya Mwaka 2004.
0 comments :
Post a Comment