WAZIRI
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Augustine Mahiga,
amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Pierre Nkurunziza wa Jamhuri ya
Burundi, kwenye Ikulu yake jijini Bujumbura.
Taarifa
ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, iliyotumwa jana
kwa vyombo vya habari, ilifafanua kwamba hatua hiyo ya Dk Mahiga, ni
utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli ambaye ndiye Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika Mashiriki, ameamua kutafuta suluhu ya kisiasa ya
migogoro iliyojitokeza baina ya Serikali na vikundi vinavyo hatarisha
amani nchini humo.
Imeelezwa
kuwa kwenye mazungumzo hayo yaliyodumu takriban saa mbili, Dk Mahiga
alimueleza Rais Nkurunziza azma ya Rais Magufuli kuamsha mazungumzo ya
kisiasa ya kuleta amani.
Dk
Mahiga pia alieleza kwamba tayari msuluhishi aliyeteuliwa na Jumuiya
hiyo, Rais Yoweri Museveni, ameanza maandalizi ya uzinduzi wa mazungumzo
hayo, yatakayofanyika Entebe, Uganda wiki ijayo Desemba 28 mwaka huu.
Waziri
Mahiga pia alieleza maoni yake kuhusu hali ya utulivu aliyoiona kwa
kipindi cha takriban saa 24 alizokuwa jijini Bujumbura na kwamba
hakusikia sauti za milipuko wala silaha zozote.
Baada
ya mazungumzo hayo, taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Nkurunziza
alimshukuru Rais Magufuli na kumhakikishia ushiriki wa Burundi, akieleza
kuwa mazungumzo ya Entebe yatasaidia kuleta amani na mshikamano baina
ya wananchi wa Burundi.
Hata
hivyo, taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Nkurunziza alisisitiza kuwa ili
mazungumzo hayo yawe na tija, ni lazima yawe na muendelezo wa ndani,
ambao yeye na Serikali yake wamekwisha yaanza.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, Rais Nkurunziza alisema ni matumaini yake kuwa
makundi yote nchini humo, wataungana kwenye mazungumzo hayo
yatakayojumuisha asasi za kiraia, kidini, vyama vya siasa na makundi
mengine, ili kujadili mustakabali wa Taifa lao kwa pamoja.
Pamoja
na kuridhia ushiriki wa Burundi kwenye mchakato huo wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Nkurunziza alieleza
kuwa yeye na Serikali yake wako tayari kushirikiana na Umoja wa Afrika
(AU) na Umoja wa Mataifa (UN) kutathmini hali ya usalama nchini mwake.
Hivi
karibuni Baraza la Amani na Usalama la AU, lilitangaza azma ya kupeleka
vikosi vya askari 5,000 nchini Burundi, kutokana na kuonekana viashiria
vya mauaji ya kimbari kama yale yaliyofanyika nchini Rwanda miaka ya
tisini.
Lakini
taarifa hiyo imeeleza kuwa, Rais Nkurunziza alisema uamuzi huo wa AU,
umewashitua wao serikalini na hata wabunge ambao ni wawakilishi wa
wananchi, waliofikia hatua ya kuhoji sababu za umoja huo kupeleka jeshi
kubwa nchini humo.
“Burundi
imekuwa ikishirikiana na Umoja wa Afrika (AU) kwenye ulinzi wa amani
ambapo ina vikosi vya askari zaidi ya elfu sita nchini Somalia na Afrika
ya Kati,” amekaririwa Rais Nkurunziza akisema.
Naye
Spika wa Bunge la Burundi, Paschal Nyabenda alieleza kusikitishwa kwake
na uamuzi huo wa AU, ambapo alimweleza Dk Mahiga kuwa misingi ya
kukataa ukabila imeainishwa kwenye katiba ya nchi hiyo na makubaliano ya
Arusha.
Spika
huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Tawala cha CNDD-FDD nchini humo,
alisema kuwa Katiba ya nchi hiyo, inalazimisha taasisi zote ziwe na
uwakilishi na pengine uwiano sawa kati ya Wahutu na Watusi.
Akielezea
muundo wa Bunge lake, Taarifa hiyo imeeleza kuwa Spika huyo alisema
Bunge hilo lina asilimia 60 kwa 40 ya uwakilishi wa Wahutu na Watusi.
Spika Nyabenda alisema kuwa Makamu wa Kwanza wa Spika, Agathon Rwasa
anatoka kwenye kabila la Wahutu na Makamu wa Pili wa Spika, Edouard
Nduwimana anatokea kwenye kabila la Watusi.
Aidha,
Naibu Spika wa Kwanza wa Bunge hilo, Agathon Rwasa ambaye pia
alishiriki kwenye mazungumzo hayo, alisema kuwa wakati umefika sasa kwa
Burundi kuangalia mbele na kwa manufaa na maendeleo ya vizazi vijavyo na
kusifu maendeleo aliyoyashuhudia nchini Tanzania ambapo alisisitiza
yamekuwepo kutokana na amani nchini humo.
Akiwa
nchini Burundi, Dk Mahiga na ujumbe wake walikutana na kufanya
mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Usalama wa Raia na Mambo ya Ndani,
ambapo alipokea taarifa ya Waziri Alain Guillaume Bunyoni, kuhusu hali
ya usalama nchini humo tangu Rais Nkurunziza alipochaguliwa na chama
chake kugombea tena nafasi ya urais Aprili mwaka huu.
Kwa
upande wake, Waziri Mahiga alisifia jitihada zilizowekwa na Wizara
hiyo, hususan kwenye upande wa ulinzi wa raia na mali zao na kusisitiza
umuhimu wa Wizara hiyo na Serikali nzima, kuwaelezea wananchi na jumuiya
za kimataifa jitihada za Serikali kuleta amani nchini humo.
Katika
ziara hiyo ya siku mbili, Waziri Mahiga pia alifanya mazungumzo na Dk
Crispus Kiyonga, Waziri wa Ulinzi wa Uganda, ambaye ameanza maandalizi
ya mazungumzo ya amani chini ya uenyekiti wa Rais Museveni wa Uganda.
0 comments :
Post a Comment