WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Eng. John Ndunguru kukamilisha uchunguzi wake na kumpatia taarifa ya maandishi juu ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma unaohusisha uuzwaji wa jengo la KIGODECO na viwanja 12 vya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambao unadaiwa kukiuka taratibu.
Ametoa agizo hilo leo mchana
(Jumatano, Desemba 30, 2015) kwenye ukumbi wa NSSF, mjini Kigoma wakati
akizungumza na viongozi na watendaji mbalimbali wa mkoa huo alipokuwa
akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkonai humo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema
anazo taarifa kuwa jengo hilo liliuzwa kwa sh. milioni 370/- pamoja na
jengo jingine la MIBOS kwa sh. milioni 50/- licha ya kupewa barua na
Mkuu wa Mkoa huo kusitisha uuzwaji wa jengo pamoja viwanja hivyo, bado
liliuzwa.
“Katibu Tawala wa Mkoa kaa na
Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa na Mhasibu na unipatie
taarifa kwa maandishi ifikapo Jumamosi hii,” alisema Waziri Mkuu huku
akishangiliwa.
“Nataka kujua nani alifanya
tathmini ya jengo, ni kwa nini jengo liliuzwa kwa thamani hiyo, je ndiyo
thamani halisi ya jengo? Ni kwa nini RC alipozuia, utaratibu
uliendelea? Je, utaratibu wa uuzaji ulifuatwa? Ni kwa nini viwanja
viliuzwa chini ya thamani,? Katibu Tawala kaa na watu wako na uniletee
hiyo taarifa kwa maandishi. Tukigundua kuna mianyamianya tutachukua
hatua za kinidhamu,” alisema.
Viongozi walioagizwa kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa ni Mkurugenzi wa
Manispaa, Eng. Boniface Nyambele; Mhandisi wa Manispaa, Eng. Boniface
William na Mhasibu wa Mapato wa Manispaa, Ndg. Bawili Mkoko.
Kuhusu uuzwaji wa jengo na viwanja, imebainika kuwa Mkuu wa Mkoa huo,
Luteni Kanali (Mst), Issa Machibya alizuia uuzaji huo kwa barua ya
tarehe 16 Juni 2015 akitaka viwanja hivyo vitumike kwa matumizi ya
manispaa na mchakato huo usitishwe hadi mwakani lakini agizo lake
lilipuuzwa na jengo likauzwa kwa sh. milioni 370 ambayo ni bei ya
kiwanja pekee.
Tuhuma nyingine zinazopaswa kuchunguzwa ni pamoja na matumizi ya sh.
milioni 809 kwa ajili ya ujenzi wa maabara.
Kiasi hicho kilitolewa kutoka kwenye fedha za miradi ya maendeleo (Capital Development Grants-CDG), Mradi wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP), Mradi wa Uendelezaji Miji (Tanzania Strategic Cities Programme –TSCP) na Miradi ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (SEDP).
Kiasi hicho kilitolewa kutoka kwenye fedha za miradi ya maendeleo (Capital Development Grants-CDG), Mradi wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP), Mradi wa Uendelezaji Miji (Tanzania Strategic Cities Programme –TSCP) na Miradi ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (SEDP).
Inadaiwa kwamba Mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi
wa idara ya mipango na fedha walitumia ujenzi wa maabara kama kigezo cha
kuchota fedha hizo bila kutoa taarifa kwa wakuu wa idara husika ambao
walikasimiwa fedha hizo.
Tuhuma nyingine ni manunuzi hewa ya vipuri (spare parts) vyenye thamani
ya sh. milioni 8 na manunuzi hewa ya stationeries yenye thamani ya sh.
milioni 4.6/-. Haya yanadaiwa kufanywa Julai 25, mwaka huu na Mkurugenzi
huyo akishirikiana na Mhasibu Mkoko.
Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam mchana huu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 30, 2015
0 comments :
Post a Comment