Clinton: Naweza kumteua Obama awe jaji
- Nkupamah Media:30,Januari 2016
Mgombea urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton amesema linaweza kuwa wazo zuri sana kumteua Rais Barack Obama kuwa jaji wa Mahakama ya Juu.
Alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mpiga kura katika mkutano wa kampeni jimbo la Iowa.
Alitakiwa aeleze iwapo baada ya kuwa Rais, anaweza kufikiria kumteua Rais
Obama kuwa jaji wa Mahakama Kuu.
Alisema rais atakayeingia madarakani ana uwezo wa kuteua majaji watatu wa Mahakama ya Juu, shirika la habari la ABC News limeripoti.
"Lo! Hilo ni wazo zuri sana. Hakuna mtu amewahi kupendekeza hilo kwangu,” alisema Bi Clinton.
“Nalipenda sana wazo hilo. Anaweza kuwa na mambo mengine kadha ya kufanya, lakini nakwambia hilo ni wazo zuri sana.”
Bi Clinton alikihutubia watu takriban 450 waliohudhuria mkutano huo.
"Ni mwerevu sana, na anaweza kutetea hoja vyema, na alikuwa profesa wa sheria, kwa hivyo amehitimu,” alisema.
“Sasa, tunahitaji kuwa na Bunge la Seneti linalodhibitiwa na chama cha Democratic ndipo aweze kuidhinishwa, kwa hivyo mtanisaidia kufanya hilo, tumekubaliana?”
Bi Clinton, alishindana vikali na Bw Obama kuwania tiketi ya kupeperusha bendera ya urais mwaka 2008 lakini akashindwa na baadaye akahudumu kama waziri wa mashauri ya kigeni wa Obama.
0 comments :
Post a Comment