Serikali
kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nauye, imelifungia kwa muda wote gazeti la kila wiki la MAWIO
linalochapishwa na kampuni ya Victoria Media Services Ltd.
Katika
tangazo lake lililotolewa kupitia gazeti la Serikali notisi namba 55 ya
Januari 15, 2016 Serikali imebainisha kuwa imechukua uamuzi huo wa
kulifungia gazeti la Mawio kwa muda wote kwa mujibu wa mamlaka iliyonayo
kupitia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229 kifungu cha 25(1).
“Mawio
linatakiwa kusimamisha uchapishaji wake kwa kipindi chote ikiwemo pia
katika vyombo vya mawasiliano vya kielektroniki kuanzia Januari 15,
2016”, ilisema sehemu ya tangazo hilo ambalo limetolewa katika gazeti la serikali, likisainiwa na waziri Nape Nauye.
Tangazo
hilo halikuweza kufafanua zaidi ni makosa gani hasa yaliyosababisha
gazeti kufungwa na kwanini adhabu iliyotolewa ni kubwa sana ukizingatia
kuwa Mawio halikuwahi kufungiwa wala kuonywa kwa kosa lolote katika siku
za wa awali.
Serikali
ilianza kulikabili rasmi gazeti la Mawio 31 Desemba, 2015 kwa barua
iliyoandikwa na msajili wa magazeti ikimtaka mhariri wa gazeti hilo
kutoa maelezo ya kwanini gazeti hilo lisifungiwe kufuatia makala zake
mbili zenye vichwa vya habari “Hosea kortini” na “Seif Rais Zanzibar” ambazo zilidaiwa kuzua taharuki.
“Nakujulisha
kwamba ofisi ya msajili wa magazeti haijaridhika na utetezi wako kwa
kuwa hujatoa uthibitisho usio na shaka juu ya madai ya makala
ulizochapisha,” ilitamka sehemu ya barua iliyosainiwa na Raphael Hokororo, kwa niaba ya msajili.
Gazeti
la Mawio ambalo huandika habari za kiuchunguzi limefuata mkondo uleule
ambao gazeti la MwanaHALISI liliufuata 30 Julai 2012 pale lilipofungiwa
kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuchapisha taarifa za uchochezi.
MwanaHALISI
lilikaa kifungoni kwa zaidi ya miaka mitatu kabla ya kurejeshwa kwa
amri ya Mahakama Kuu mwezi Agosti, 2015 kufuatia Mkurugenzi wa kampuni
ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea kufungua kesi, akipinga kufungiwa kwa gazeti hilo.




0 comments :
Post a Comment