WANASIASA WAKWAMISHA SHUGHULI ZA URAGHABISHI WILAYA YA SHINYANGA VIJIJINI

Mchungaji wa kanisa la Umoja wa Makanisa ya Ubatizo  Lucas Machibya akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani ) kuhusu baadhi ya shughuli za uraghabishi katika kijiji cha Pandagichiza
 
Na Krantz Mwantepele ,Shinyanga
Si mara nyingi viongozi wa kidini hujihusisha
moja kwa moja na harakati za kisiasa ila wamekuwa mstari wa mbele kukemea
matendo yanayofanywa na wanasiasa. Hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya ila kutokana
na nafasi yao katika jamii, hususani kuwaongoza waumini wao kwenda mbinguni.
 
Hata hivyo, hii haimaanishi hakuna
kabisa viongozi wa dini waioamua kujiingiza katika harakati za siasa ili kuleta
maendeleo ya watu kwa haraka na ufanisi. Mchungaji Lucas Machibya ni mmoja kati
ya viongozi wachache wa dini wanaoingia katika siasa.
Huyu ni mchungaji wa kanisa la Umoja
wa Makanisa ya Ubatizo lililopo katika kijiji
cha Pandagichiza chenye wakazi wanaokadiriwa 2,481, idadi kubwa ikiwa ni ya
wanawake wanaokadiriwa kufikia 1,476. Hiki ni moja ya vijiji vilivyopo wilaya
ya Shinyanga Vijijini, jimbo la Solwa.
Machibya ni mmoja wa wachungaji
waraghbishi toka mkoa wa Shinyanga ambao uraghbishi wao umepelekea wananchi
kumchagua kuwa mwenyekiti wa kijiji. Kujibainisha kwake kama mtu mwenye uwezo
wa kusimamia anachokiamini na kushawishi wananchi kutambua majukumu na haki zao
na jinsi ya kuzidai vimekuwa nguzo yake kubwa ya kukubalika.
Kama walivyo wananchi wengi wa kijiji
chake, yeye ni mkulima mdogo ambaye pia ni mwanachama wa Mtandao wa Wakulima
Wadogo Tanzania (MVIWATA). Kupitia mwaliko wa mkulima mwenzake, Elizabeth
Edward, Machibya amefanikiwa kupata maarifa ya uraghbishi na jinsi ya kufanya
uraghbishi; uwezo wa kuwashawishi na kuwahusisha ama kuwachokoza watu ili
waweze kujitambua na kutojiona wao ni wa jamii ya chini.
Sifa iliyomfanya aalikwe kwenye
mafunzo ya uraghbishi ni uwezo wake wa kuhoji mambo mbalimbali pasipo kukata
tamaa kama anavyosema mwenyewe:
“Mimi ni mtu wa kuhoji vitu na si mtu
wa kuridhika ama kukaa kimya n’napoona kuna jambo sijalielewa. Kwa kweli yale
mafunzo yalinifanya kujiona mtu tofauti sana nikijilinganisha na nilivyokuwa
awali. Nilijihisi tayari nimekuwa mtaalamu wa masuala ya uwajibikaji na utawala
bora.”
Kwa kuwa wao ni wakulima, walianza uraghbishi
wao kwa kutaka kujua nini kinaendelea kuhusu bei ya pamba. mchungaji Machibya anaeleza
ilivyokuwa:
“Kule tulifundishwa jinsi ya kuuliza
maswali. Na cha kwanza tulichotaka kujua ni kwa nini bei ya zao letu la pamba
imeshuka sana. Hili tuliliuliza sisi sote, mimi na waraghbishi wengine.”
Hawakuishia hapo tu bali wakaanza pia kufuatilia
mapato na matumizi ya fedha za kijiji toka kwa viongozi wao. Walifanya hivyo
kwa kuwatembelea ofisini na kuomba kupatiwa taarifa hizo na pia walitaka
kufanyika mikutano ya hadhara. Baada ya harakati hizo kushika kasi, iliwabidi
waongeze watu wengine zaidi kwa kuwatembelea majumbani kwao na kuwaraghbisha.
“Mchungaji aliomba kunitembelea
nyumbani na alipofika alinipatia elimu. Kimsingi, alitaka nijitambue kwa kujua
wajibu na haki zangu. Alinitaka nisiogope kuuliza maswali kwenye mikutano kwa
kuwa tuna uhuru wa kufanya hivyo. Nikajua kuwa nina wajibu kuuliza na kujua mapato
ya fedha za kijiji na na matumizi yake kuwa hiyo ni haki yangu,” anaeleza Bw. Daudi
Denis toka kijiji cha Pandagichiza.
Baadhi ya waraghabishi wa kijiji cha Pandagichiza wakiwa na waandishi wa habari za mtandaoni katika moja ya jengo la jiko  la shule ya msingi Pandagichiza ambalo limetoakana na juhudi zao za uraghabishi 
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment