Waziri Simbachawene Amsimamisha Kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma

Nkupamah media


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mh. George Simbachawene amemvua madaraka Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, Bw. Augustino Kalinga kufuatia kuruhusu ofisi yake kuwachangisha wazazi michango ambayo serikali imezuia katika kutoa elimu ya msingi bila malipo.

Mh. Simbachawene alifikia uamuzi huo jana mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali baada ya kugundua kuwa manispaa ya Dodoma imesambaza barua kwa walimu wakuu wa shule za msingi ambazo zimeagiza kuwatoza wazazi michango ya maji, umeme na mlinzi ambayo imekatazwa na serikali.

Alisema kuwa Bw. Kalinga amevuliwa madaraka yake baada ya kubainika kuwa ameshindwa kuwasimamia watumishi walio chini yake hadi kusababisha kuandika barua na kusambaza kwa walimu wakuu wa shule za msingi katika manispaa ya Dodoma ambayo inatofautiana na maelezo ya serikali yaliyopo kwenye mwongozo.

Mbali na Kapinga, Waziri Simbachawene pia alimsimamisha Ofisa elimu vifaa na takwimu-wa msingi katika Manispaa hiyo, Josephine Akimu kwa kudharau maelekezo ya kiongozi wake na kusaini barua kwa niaba ya mkurugenzi huku akitumia jina la Ofisa Elimu, Scola Kapinga ambaye pia amepewa onyo kali.

Sababu za kuwavua madaraka watumishi hao ni kutokana na kuandika barua yenye kumbukumbu HMD/ED/50/2/VOL 11/61 ya Januari 17, mwaka huu iliyosambazwa kwa walimu wakuu wote wakitakiwa kuchangisha michango katika shule za msingi wakati Serikali ilishazuia.

Barua hiyo ilikuwa na maelekezo ya kuwataka walimu wakuu kuchangisha michango ya maji, mlinzi na umeme, jambo ambalo lilimfanya waziri kufanya safari ya kushtukiza Shule ya Msingi Dodoma Makulu, na kujionea michango hiyo lakini akabaini kulikuwa na barua za maelekezo kutoka ofisi ya mkurugenzi.

“Ieleweke kuwa uchangiaji ulioelekezwa katika barua ya mkurugenzi ni kinyume na maelekezo ya Rais John Magufuli, sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ibara ya 3.1.5 na ilani ya Uchaguzi ya CCM ibara ya 52 (a) ya mwaka 2015 ya kutoa elimu bure bila ya malipo,” alisema Simbachawene.

Alisema maelekezo ya maofisa hao ni kinyume na mwongozo namba DB.297/507/01/39 wa Desemba 28, 2015 uliotolewa na ofisi ya Tamisemi kwa makatibu Tawala wa mikoa, wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri zote kuhusu matumizi ya fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule za msingi za Serikali katika kutekeleza kaulimbiu ya elimu bure.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment