Mwanasheria Mkuu wa Serikali Asema Rais Magufuli Hana Mamlaka Kikatiba Ya Kuingilia Mambo Ya Zanzibar

nkupamah media:


Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju amesema Rais John Magufuli hana mamlaka ya kikatiba ya kuingilia masuala ya Zanzibar ukiwamo uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20.

Hii ni kauli ya pili kutolewa ndani ya wiki moja ikieleza hali hiyo, baada ya ile ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Luvuba aliyoitoa wiki iliyopita baada ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam.

Akizungumza bungeni juzi, Masaju alisema: “Katiba ya Zanzibar si ya Muungano, masuala ya ulinzi na usalama ndiyo ya Muungano na ndiyo sababu ulinzi umeimarishwa visiwani humo kuhakikisha nchi hiyo inakuwa salama."

Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akifafanua mambo mbalimbali yaliyozungumzwa na wabunge wakati wa mjadala wa mwongozo wa mpango wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/17 na Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.

Tangu kuibuka kwa mgogoro Zanzibar watu wa kada mbalimbali wamekuwa wakisema mwarobaini wa mgogoro huo kwa kutumia jitihada za ndani, ufanywe na Rais Magufuli baada ya jitihada za viongozi wa kisiasa visiwani kukwama.

Mgogoro huo, ambao umekuwa kawaida kuibuka kila baada ya Uchaguzi Mkuu, uliibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha kufuta matokeo Oktoba 28 na baadaye kuuitisha upya, kitendo ambacho CUF inakipinga.

Tangu wakati huo, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd na marais wa zamani wa Zanzibar, Dk Salmin Amour, Ali Hassan Mwinyi na Amani Karume wamekuwa kwenye mazungumzo ambayo hayakuzaa muafaka.

“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uwepo wa Serikali mbili. Hizi Serikali uwepo wake ni Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar. Ukisoma Ibara ya nne ya Katiba si tu kwamba inaweka mgawanyo wa madaraka katika mihimili mitatu ya Dola, bali inaweka mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.”


Ibara ya 4 ya Katiba inasema (1) Shughuli zote za Mamlaka ya nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji, vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki na pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.

(2) Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni Idara ya Mahakama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Idara ya Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge na Baraza la Wawakilishi.

(3) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na mambo ya Muungano kama alivyoorodheshwa katika nyongeza ya Kwanza iliyoko mwishoni mwa Katiba hii, na pia kutakuwa na mambo yasiyo ya Muungano ambayo ni mambo mengine yote yasiyo ya Muungano.

(4) Kila chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na kutekeleza majukumu yake kwa kufuata masharti mengine yaliyomo katika Katiba hii.

Masaju alisema Katiba ya Zanzibar ndio inayozaa ZEC.

“Kile ambacho baadhi ya wabunge wamekisema hapa ni kama kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia mamlaka ya Zanzibar na tafsiri yake ni kama unataka kuleta hoja ya kujenga Serikali moja,” alisema.

Alisema kufanya hivyo ni kuvunja Katiba ya Muungano na ya Zanzibar na Serikali haiwezi kufanya hivyo
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment