Jeshi la Polisi mkoani Singida linawashikilia vijana wanne kwa tuhuma za kupatikana na misokoto 40 ya bangi kinyume cha Sheria za nchi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa, Thobias Sedoyeka aliwataja waliokamatwa kuwa ni Yusuph Shaban (22) kinyozi mkazi wa Minga mjini Singida, Jackson Francis mkulima mkazi wa Mnung’una Singida, Hamisi Rashid (20) mkulima mkazi wa Da es Salaam na Kenedy Godfrey (20) mkulima mkazi wa Tanga.
Kamanda Sedoyeka aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa tukio hilo lilitokea Feb mosi mwaka huu majira ya saa 3.30 usiku wakati wahusika walipokutwa na askari wa doria wakiwa wamekaa kwenye saluni moja anakofanya kazi Yusuph Shaban; hivyo kuwatilia shaka.
Alisema kuwa baada ya kuwatilia shaka, askari polisi hao waliwafanya upekuzi ndani ya saluni hiyo ambapo walifanikiwa kukuta jumla ya misokoto 40 ya bangi baadhi ikiwa imefichwa ndani ya mfuko wa plastiki chini ya redio na mingine kwenye mifuko ya suruali za watuhumiwa.
Alisema kuwsa watuhumiwa bado wanashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi ili kubaini mtandao mzima wa biashara hiyo ya bangi pamoja na madawa mengine ya kulevya na kwamba mara baada ya uchunguzi kukamilika watafikishwa mahakamani.
Kamanda Sedoyeka ametoa mwito kwa jamii mjini hapa kuacha biashara na matumizi ya madawa hayo ya kulevya kwa kile alichodai yamekuwa chanzo kikubwa cha uhalifu na kusababisha matatizo ya kiafya na wakati mwingine vifo kwa watumiaji; hasa vijana.
Hata hivyo, wakati jeshi hilo likijinasibu kukamata vijana hao, wakazi mbalimbali wa mji huu wamedai kuwa mara zote polisi wamekuwa wakikamata watumiaji tu na kuwaacha wauzaji na wasambazaji wa madawa hayo ambao ndio chanzo kikuu cha tatizo hilo.


0 comments :
Post a Comment