Wanamichezo mbalimbali mkoani Singida, wameshauriwa kujiepusha na matumizi ya viroba (pombe) na madawa ya kulevya ili kujijengea mazingira mazuri katika kufikia malengo yao ambayo ni pamoja na kujipatia ajira au kujiajiri.
Wito huo umetolewa na Afisa michezo mkoa wa Singida, Henry Kapera wakati akizungumza kwenye hafla ya kuipongeza timu ya Singida United F.C kwa kufanikiwa kupanda daraja la kwanza msimu ujao.
Akifafanua, alisema matumizi ya viroba na madawa ya kulevya ni sumu mbaya ambayo mtumiaji awe mwanamichezo au mtu yoyote, hataweza kufikia ndoto au malengo yake.
“Mafanikio haya ambayo mmeyapata yanayoashiria kuwepo kwa dalili kubwa mkoa wa Singida ukarejea ligi kuu, mna kazi kubwa zaidi kufikia lengo hilo, niwasihi msijiingeze kwenye matumizi ya viroba wala madawa ya kulevya ili muweze kufikia lengo lenu na la mkoa pia,” alisema Kapera.
Aidha.afisa michezo huyo, amewataka waendelee kudumisha nidhamu ndani na nje ya uwanja na wakati wote, wazingatie yale yote wanayoelekezwa na mwalimu wao (kocha).
Kwa upande wa mmiliki wa Singida United na mchimbaji maarufu wa madini mkoani hapa,Yusuph Mwandami, alisema kimsingi timu ya Singida United ni ya wakazi wa mkoa wa Singida,na inafanya kazi ya kuutangaza mkoa kupitia mchezo wa soka.
“Nitumie fursa hii kuiomba serikali ya mkoa wa Singida na wadau mbalimbali,tushirikiane pamoja kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri katika kazi hii ngumu inayowakabili ya mikiki mikiki ya ligi daraja la kwanza ili iweze kufikia malengo yake,” alisema Mwandami ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi(CCM) mkoa wa Singida.
Alisema kuwa kwa upande wake amejipanga vizuri kwa maana ya kuiandaa timu vizuri iweze kushiriki ligi daraja la kwanza bila matatizo.Usajili pia utakuwa wa ngazi ya ligi darala la kwanza.
“Nitoe wito kwa wapenzi wa michezo na hasa Singida United,kushiriki kwa hali na mali na sote tuimbe wimbo moja nao ni timu yetu kufanya vizuri na kufanikiwa kucheza ligi kuu,” alisema.
Na Nathaniel Limu, Singida

Kocha wa Singida United Fulgence Novatus,akitoa nasaha zake kwenye halfa ya kuipongeza timu hiyo kupanda daraja la kwanza msimu wa 2016/2017.

Baadhi ya wachezji wa timu ya Singida United waliohudhuria hafla iliyofana ya kupongezwa kupanda daraja la kwanza msimu wa 2017/2018.

Katibu wa timu ya soka ya Singida United F.C.Abrahamani Sima,akisoma taarifa yake kwenye hafla ya kuipongeza Singida United kupanda daraja la kwanza msinu wa 201/2017.Sima alisema timu yao inahitaji zaidi ya shilingi milioni 200,ili iweze kushiriki vema ligi hiyo yenye ushindani mkali.

Afisa michezo na burudani mkoa wa Singida, Henry Kapera,akizungumza kwenye hafla ya kuipongeza timu ya Singida United kupanda daraja la kwanza katika msimu wa 2016/2017.Kapera pamoja na kuipongeza timu hiyo,aliwataka wachezaji kujiepusha na matumizi ya viroba na madawa ya kulevya,ili waweze kutimiza ndoto yao ya kucheza ligi kuu msimu 2017/2018.

Mmliki wa timu ya Singida United na mchimbaji maarufu wa madini mkoani hapa,Yusuph Mwandami,akitoa nasaha zake kwenye hafla ya kuipongeza timu hiyo kwa hatua yake ya kupanda daraja la kwanza msimu wa 2016/2017.Mwandami amewataka wakazi wa mkoa wa Singida,kuisaidia kwa hali na mali timu yao hiyo iweze kufuzu kucheza ligi kuu msimu wa 2017/2018. (Picha na Nathaniel Limu)



0 comments :
Post a Comment