WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) aende Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kufanya upya
tathmini na kukagua ugawaji wa viwanja 843 kwenye manispaa hiyo.
Waziri
Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo jana (Jumatatu, Machi 14, 2016) wakati
akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Mayunga mjini Bukoba.
Alifikia
hatua hiyo baada ya wananchi kubeba bango lenye ujumbe kuelezea
kutopewa viwanja hivyo vilivyopimwa na Manispaa ya Bukoba.
Viwanja
hivyo vilipimwa na kugawiwa kwa wananchi ambao baadhi yao baada ya
kulipa fedha, hawajapewa viwanja hivyo ikiwa ni takriban miaka zaidi ya
10.
Akiwa
katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kagera, Waziri Mkuu
alilazimika kumpandisha jukwaani Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo,
Bw. Wallace Karia ili atoe maelezo ya nini kimekwamisha wananchi kupewa
viwanja hivyo.
Katika
maelezo yake, Bw. Karia alisema mwaka 2003, vilitengwa viwanja 843,
kati ya hivyo 352 vilikuwa eneo la Kyabitembe, 137 Ihungo na Rwome na
vingine 132.
Bw.
Karia ambaye hana muda mrefu tangu ahamishiwe katika manispaa hiyo,
alisema kumbukumbu za ofisi zinaonesha kuwa viwanja 182 ndio wahusika
hawajapewa, na viwanja vingine 85 vilikuwa havijapimwa eneo la
Kilimahewa na Kashai, huku kukiwa na vingine 5,000 vya mradi.
Aliongeza
kuwa walitarajiwa kuwalipa wananchi hao katika mwaka wa fedha 2016/17;
kauli ambayo ilisababisha kelele kutoka kwa wananchi waliohudhuria
mkutano huo wa Waziri Mkuu.
Kutokana
na hilo, Waziri Mkuu aliingilia kati na kumueleza Mkurugenzi huyo kuwa
kelele hizo zinaashiria kuwa watu hao hawajaridhishwa na majibu yake.
Alisema
anafahamu kuwa mkurugenzi huyo na meya ni wapya, lakini akawaagiza
ndani ya mwezi mmoja, kufanya mapitio ya viwanja hivyo 843, na hasa watu
182 ambao hawajapatiwa viwanja wahakikishe wanawapatia kwa sababu
viwanja vipo.
“Rais
mstaafu alikuja hapa na kupewa kilio cha kupunjwa fedha. Najua wakati
huo mtasema ninyi hamkuwepo. Wewe (MD) na Meya wako mkae na kupitia
mikataba na mafaili. Nyie na mkoa mkae pamoja na kujua vile viwanja
vilivyochukuliwa na JWTZ. Nitamleta CAG hapa, ndani ya mwezi mmoja
afanye mapitio ya viwanja tu,” alieleza Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya wananchi.
Katika
mkutano huo, Waziri Mkuu pia aliwahakikishia wakazi wa Manispaa ya
Bukoba kuwa watalipwa fidia zao baada ya kukubali kupisha ujenzi wa
mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh. bilioni 31.
Waziri
Mkuu aliendelea na ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera kwa kutembelea
wilaya za Misenyi na Karagwe na leo atakuwa wilayani Ngara.


0 comments :
Post a Comment