Hatimaye hukumu ya kesi iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Saed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo akidaiwa kumtolea lugha ya matusi Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kindononi imefika tamati.
Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu katika Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam amesema, mahakama hiyo imemtia hatiani Kubenea na kumpa adhabu ya kutofanya kosa linalofanana na hilo ndani ya miezi mitatu.
“Mahakama imejiridhisha kuwa, hilo ni kosa lako la kwanza na kwa kuzingatia nia uliyoenda nayo ya kutatua mgogoro wa wafanyakazi, lakini pia imejiridhisha kwa kutumia ushahidi wa upande wa mashtaka, hivyo inakutaka usifanye kosa linalofanana na hilo na kuletwa tena mahakamani” amesema hakimu.
Amesema kuwa, kila upande upo huru kukata rufaa endapo wataona kuwa hukumu iliyotolewa hawaridhiki nayo, ambapo pale pale jopo la mawakili wa Kubenea likiongozwa na Peter Kibatala, waliiambia mahakama kuwa wanaweka nia ya kukata rufaa kwa sababu ushahidi uliotumika kuhukumu umeacha mashaka mengi.
Nje ya mahakama Kubenea amewaambia waandishi wa habari kuwa yeye bado ni Mbunge wa Ubungo na wananchi wa Ubungo wasiwe na hofu kwani hizo ni harakati za siasa.
John Mallya, mmoja wa mawakili aliyekuwa akimtetea Kubenea amesema kuwa, mahakama haikupaswa kuegemea kwenye ushahidi wa polisi peke yake kufikia uamuzi huo kwa kuwa polisi wasingeweza kumpinga Makonda.
Amehoji ni kwanini upande wa Jamhuri haukuleta mfanyakazi hata mmoja kutoa ushahidi.
Kesi hiyo ilifunguliwa tarehe 15 Desemba mwaka jana baada ya viongozi hao wawili kutofautina kwenye Kiwanda cha nguo cha TOOKU kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam tarehe 14 Desemba mwaka jana ambapo Kubenea alikamatwa na polisi kwenye eneo hilo kwa amri Makonda.
Tukio hilo lilitokea kukiwa na mgomo wa wafanyakazi zaidi ya 1800 wa kiwanda hicho ambao walimpigia mbunge huyo aende kutatua mgogoro huo.
Kubenea alifika katika eneo hilo saa 6 mchana na kukutana na wafanyakazi kusikiliza kero zao za muda mrefu.
Kisha aliamua kuondoka na viongozi wa wafanyakazi hao na kufanya kikao na menejimenti ya kiwanda hicho kuanzia saa 7 hadi saa 9.
Ilipofika saa 10:30, Makonda alifika na kupata taarifa kwa muafaka uliofikiwa kati ya Kubenea, menejimenti na viongozi wa wafanyakazi.
Alitoa amri wafanyakazi wakusanyike, akaawaambia kesho atafika huko na Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Kazi na Ajira, na Waziri wa Afya Wanawake, Jinsia na Watoto.
Baada ya kutoa maagizo hayo, Makonda alimzuia Kubenea kuhutubia na kuaga wananchi aliokuwa nao tangu mchana, kutokana na hali hiyo (Kubenea) alisema ni vema aseme neno, ndipo mvutano ulipoanza.
Makonda alimuru mkutano ufungwe lakini wafanyakazi hawakutawanyika eneo hilo, alipoona hivyo aliamrisha Polisi wamkamate Kubenea ambapo sintofahamu iliongezeka.
0 comments :
Post a Comment