Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Viongozi
wa Kamati ya Siasa na Wizaya za Diani, Mfenesini pamoja na Mkoa wa
Magharibi katika mkutano wa kupongezana baada ya ushindi mkubwa kwenye
uchaguzi Mkuu uliopita hapo Tawi la CCM Mbweni nje kidogo ya mji wa
Zanzibar.
Kulia
ya Balozi Seif ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi Bibi
Aziza Ramadhan Mapuri na Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa CCM
Wilaya ya Dimani Nd. Abdulla Shunda.
Baadhi
ya wajumbe wa Kamati za Siasa za Wilaya za Dimani, Mfenesini na Mkoa wa
Magharibi wakifuatilia hotuba ya Mjumbe wa Kamat Kuu ya CCM Taifa ambae
pia ni Mlezi wa Mkoa wa Magharibi Kichama Balozi Seif.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi
Seif Ali Iddi alisema kazi kubwa inayowakabili Viongozi na Wanachama wa
CCM kwa wakati huu ni kuzifanyia kazi changamoto zote zilizojitokeza
katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita ili kazi iwe rahisi wakati
chama hicho kitapoingia kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Alisema
mambo yote yanayopaswa kufanywa ili kujenga mazingira bora zaidi ya
ushindi ni lazima yakatekelezwa ndani ya kipindi hichi cha miaka minne
iliyoanza hivi sasa.
Balozi
Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati za
Siasa za Wilaya ya Dimani, Mfenesini pamoja na Mkoa wa Magharibi katika
kikao cha kuwapongeza kufuatia ushindi wa kishindo uliopata Mkoa huo
katika nafasi za Ubunge,Uwakilishi na Udiwani mkutano uliofanyika kwenye
Tawi la CCM Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema
wakati huu ni wa kurekebisha na kujenga nyumba ya ushindi wa mwaka 2020
na kusisitiza uzikwaji wa makundi yote yaliyojichomoza ndani ya chama
na kupelekea wakati mgumu wa kujenga nguvu za ushindi kwenye Uchaguzi
kwa baadhi ya Majimbo na Wadi.
Balozi
Seif alieleza kwamba wapo baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi
hasa Vijana waliodharau kujitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi Mkuu wa
Mwezi Oktoba na hata ule wa marejeo na kusababisha upunguzaji wa kura za
chama hicho katika baadhi ya Majimbo na kusababisha ushindi hafifu
kwenye Majimbo hayo.
Mjumbe
huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwakumbusha
Viongozi wa Kamati za Siasa akiwa Mlezi wa Mkoa huo Kichama kuhakikisha
wanawaelimisha Vijana wao umuhimu wa kujua thamani ya kura katika
muelekeo wa kukijengea mazingira bora ya uwajibikaji Chama chao.
Hata
hivyo Balozi Seif aliwashukuru na kuwapongeza Viongozi hao wa Kamati za
Siasa za Mkoa wa Magharibi na Wilaya zake kwa kazi ngumu waliyoifanya
katika kukipatia ushindi chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi wa marejeo
uliofanyika Tarehe 20 Machi mwaka 2016.
Balozi
Seif alisema katika uchaguzi huo wa marejeo Chama cha Mapinduzi
kilifanya vyema baada ya kujirekebisha kutokana na kasoro na
changamoto mbali mbali zilizowahi kujichomoza kwenye uchaguzi wa Mwezi
Oktoba mwaka 2015 ambapo kasoro hizo zilipelekea Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar kufuta uchaguzi na matokeo yake yote.
“
Nimepata faraja kubwa kama mimi ni mlezi wa Mkoa wa Magharibi Kichama
kutokana na ushindi mliopata kwenye Majimbo na Wadi zenu licha ya
kupoteza Jimbo moja kwa upande wa Ubunge ”. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha
kwamba mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2015 ulikumbwa na changamoto
nyingi lakini zilipata ufumbuzi kufuatia mshikamano mkubwa uliopo baina
ya Viongozi na wanachama wao Matawini na Majimboni.
Aliwataka
Viongozi na Wanachama wa Mkoa na Wilaya hizo kutokubali kubweteka au
kulemaa kwa ushindi walioupata na badala yake wajipange vizuri zaidi
ili kazi ya kukipatia fursa chama chao kuendelea kuongoza Dola iwe
rahisi wakati utakapowadia.
Akizungumzia
ahadi zilizotolewa na viongozi wa juu wakati wa kampeni za uchaguzi
Balozi Seif aliwaomba Viongozi wa Wilaya na Mikoa kuziratibu ahadi zote
ili kuwapa faraja Wananchi waondokane na mawazo ya kupewa ahadi hewa
zisizotekelezeka.
Alisema
Chama cha Mapinduzi kinakusudia kuingia kwenye uchaguzi ujao wa mwaka
2020 kikiwa hakina dhima ya ahadi zilizobakia katika utekelezaji
unaotarajiwa kufanyika ndani ya kipindi hichi cha miaka minne
iliyobakia.
Balozi
Seif aliwakumbusha Viongozi walioteuliwa Majimboni na Kwenye Wadi
kutumia lugha ya kiungwana wakati wa kuwahudumia wananchi wao ili ile
kiu ya matarajio yao waliyoionyesha kwa kumchaguwa kuwaongoza ipate
kukamilika.
Alionya
kwamba tayari wapo baadhi ya Viongozi waliochaguliwa na wananchi
wameshaanza tabia ya kuzima au kutopokea simu kutoka kwa wananchi wao
kwa visingizio vya kuweko kwenye vikao au Mikutano nyeti.
Alisema
huo ni mwanzo mbaya unaokaribisha kuanza kwa tabia ya kupikiana
majungu, vikundi na fitina ambapo mambo yote hayo kwa sasa wakati wake
umekwishwa mara tu baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
Mapema
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi Bibi Aziza Ramadhan
Mapuri alisema uchaguzi wa marejeo katika mkoa huo umefanyika kwa
mafanikio makubwa yaliyotokana na mshikano uliowekwa kati ya Viongozi na
Wanachama wao.
Bibi
Aziza alisema Majimbo 13 kwa nafasi za Uwakilishi na wadi 26 kwa nafasi
za Udiwani zimechukuliwa na wagombea wa Chama cha Mapinduzi ukitoa
Jimbo la Mwanakwerekwe kwa upande wa Ubunge lililochukuliwa na chama cha
Upinzani.
Wakichanga
kwenye kikao hicho cha kupongezana baadhi ya wajumbe wa Kamati za Siasa
za Mkoa wa Magharibi na Wilaya zake mbili waliuomba Uongozi wa juu wa
chama pamoja na Serikali kutowaonea haya watu wenye sura mbili katika
utekelezaji wa dhamana zao makazini.
Walisema
jamii imekuwa ikishuhudia hujuma nyingi zinazofanywa na baadhi ya
watendaji hasa Serikalini wakati wanapotekeleza majukumu yao bila ya
hata kukemewa wala kuchukuliwa hatua za kisheria jambo ambalo
linaondosha imani kwa wale walio chini yao.




0 comments :
Post a Comment