Kiungo mkabaji kutoka Kenya, Victor Wanyama anayekipiga katika klabu ya Southampton ya England anataraji kujiunga Tottenham baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa klabu hiyo inayoongozwa na meneja wake wa zamani inamuhitaji.
Mitandao mbalimbali ya michezo barani Ulaya imeripoti kuwa tayari Southampton wamethibitisha uhamisho huo na kinachosubiriwa ni Wanyama kufanyiwa vipimo kisha kuhamia Tottenham.
Wanyama ambaye amesalia na mkataba wa mwaka mmoja na klabu yake ya sasa, Southampton, uhamisho wake wa kuhamia Tottenham unatajwa kufikia kiasi cha Pauni Milioni 12.
Kama Wanyama usajili wake ukikamilika basi kuanzia msimu ujao ataanza tena kuonekana katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya mara ya mwisho kucheza michuano hiyo mikubwa Ulaya kwa vilabu kipindi akiwa na Celtic kabla ya kuhamia Southampton.