Fainali ya mashindano makubwa ya tenesi ya Wimbledon kwa upande wa wanaume imekamilika leo baada ya jana mwanadada, Serena Williams kutwaa taji hilo kwa upande wa wanawake, kwa upande wa wanaume Mwingereza, Andy Murray ametwaa taji hilo.
Murray amefanikiwa kushinda taji la Wimbledon baada ya kumfunga Mcanada, Milos Raonic kwa seti 6-4, 7-6(7-3) na 7-6(7-2).
Ushindi wa taji hilo umemfanya Murray kuwa mchezaji wa tenesi wa 12 katika historia ya Wimbledon kushinda taji hilo mara mbili lakini pia kuwa taji lake kubwa la tatu ‘Grand Slam’ katika historia yake ya kucheza tenesi.
Mchezo huo wa fainali ulihudhuriwa na watu mbalimbali mashuhuri akiwepo Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron aliyekuwa na mama yake, Mary na kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ambaye pia anatajwa kuwa shabiki wa Murray.