Balozi
wa Tanzania Nchini Marekani Balozi Wilson Masilingi akisalimiana na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Vuga
kubadilishana naye mawazo ukiwemo mchakato wa uchaguzi mkuu.
Balozi
Seif akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Tanzania
Nchini Marekani Balozi Wilson Masilingi Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Balozi
Masilingi alimthibitishia Balozi Seif juhudi atakazochukuwa katika
kuieleza Dunia hali halisi ya Tanzania ilivyo hivi sasa baada ya
kumalizika kwa uchjaguzi Mkuu.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba
Uhusiano wa Kidiplomasia uliopo kati ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
na Marekani sambamba na Zanzibar utaendelea kuwepo kama kawaida kwa
faida ya Wananchi wa pande mbili husika.
Alisema
kinachohitajika kwa sasa katika kukabiliana na changamoto
zinazojitokeza kwenye miradi ya Kiuchumi na Maendeleo ni kupatiwa
Taaluma kwa watendaji wa Taasisi na mashirika ya Misaada kuelewa vyema
mazingira halisi ya Tanzania hasa Zanzibar kisiasa na ustawi wa jamii.
Balozi
Seif Ali Iddi alieleza hayo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
wakati akibadilishana mawazo na Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania Nchini Marekani Balozi Wilson Masilingi anayefanya kazi zake
Jijini Washington DC.
Alisema
wapo watendaji wa baadhi ya Mashirika na Taasisi za Misaada ya
Maendeleo wanaofanya kazi Nchini ambao hupata ushawishi unaombatana na
utashi wa watu wenye nia isiyo sahihi kwa maendeleo ya Wananchi na
matokeo yake kuisumbua jamii ya walio wengi.
“
Uhusiano wetu na Marekani bado ni mzuri na utaendelea vyema, lakini
kinachohitajika kwa Taasisi nyengine za Misaada ni kupatiwa Taaluma ya
kuyaelewa mazingira halisi ya Tanzania hasa ule upande wa Zanzibar ”.
Alisema Balozi Seif.
Balozi
Seif alisema Mashirika na Taasisi zinazotoa misaada hapa Nchini lengo
lake kuu ni kuimarisha uhusiano kupitia Balozi zake na kamwe si
sindikizo la baadhi ya watendaji wake kutaka kufanya wanavyotaka
kibinafsi.
Akizungumzia
suala la uchaguzi wa marejeo Zanzibar uliofanyika Tarehe 20 Machi mwaka
huu, Balozi Seif alimueleza Balozi Masilingi kwamba kazi inayowakabili
Watanzania hivi sasa ni kujielekeza zaidi katika kuimarisha miradi ya
kiuchumi badala ya kuendeleza porojo.
Alisema
Tume ya Uchaguzi Zanzibar { ZEC } ilifikia maamuzi ya kufuta Uchaguzi
na matokeo yake yote kutokana na hitilafu kadhaa zilizojitokeza zikiwemo
za kuchafuliwa kwa matokeo makusudi kwenye vituo mbali mbali.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi Wilson Masilingi kwa
juhudi kubwa anazoendelea kuzichukuwa za kuieleza Dunia hali halisi ya
mazingira ya Tanzania ilivyo kiuchumi na kisiasa.
Alisema
jitihada za Balozi Masilingi na umakini wake katika kutekeleza majukumu
yake ndizo zilizopelekea kubadilishwa kituo kidogo cha kazi na
kuhudumia kituo kikubwa zaidi.
Mapema
Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Marekani Balozi
Wilson Masilingi anayefanyia kazi zake Jijini Washington DC aliwashukuru
Viongozi na Wananchi wa Tanzania Bara pamoja na Zanzibar kwa kumaliza
zoezi zima la uchaguzi katika misingi ya amani na utulivu.
Alisema
Watanzania walio nje ya Nchi hasa katika Majimbo mbali mbali ya
Marekani walikuwa katika mazingira magumu pale waliposikia uchaguzi Mkuu
wa Zanzibar umefutwa pamoja na matokeo yake yote hasa ikizingatiwa
historia ya Zanzibar katika medani ya Kisiasa.
Balozi
Masilingi alieleza kwamba faraja ya Watanzania hao ilirejea kama
kawaida pale Viongozi wa Kitaifa walipokuwa wakitoa Taarifa rasmi za
Serikali kuhusu yaliyojitokeza pamoja na ufafanuzi wa kina wa Viongozi
wa Taasisi zinazohusika na usimamizi wa Uchaguzi { yaani tume }.
0 comments :
Post a Comment