SERIKALI
imesema muda si mrefu inatarajia kuanza kutekeleza miradi ya maendeleo
kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia 100, kutokana na washirika wa
maendeleo kuanza kupunguza ufadhili na misaada katika miradi hiyo.
Hayo
yameelezwa jana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, wakati
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa(CCM),
aliyetaka kujua ni lini serikali itaacha kutegemea wafadhili katika
kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ngalawa
pia alitaka kujua ni lini serikali itajenga miundombinu ya umwagiliaji
nchi nzima ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji. Lwenge alisema kwa sasa
washirika wa maendeleo wamepunguza kusaidia miradi ya maendeleo, jambo
ambalo limeifanya serikali kujipanga kuanza kutekeleza miradi ya
maendeleo kwa fedha za ndani kwa asilimia 100.
Akijibu
swali la pili la nyongeza la Ngalawa, Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Isack Kamwelwe alisema zipo hekta milioni 29.4 za
kutekeleza miradi ya umwagiliaji kwa kuziwekea miundombinu na kwa mwaka
huu, hekta milioni 12 zitajengwa miundombinu ya umwagiliaji.
Katika
swali la msingi, Ngalawa alitaka kujua mpango wa serikali wa
kuliendeleza bonde la Mto Ruhuhu lililopo katika kata ya Ruhuhu wilaya
ya Ludewa, ambalo ni eneo muhimu sana na linaweza kuzalisha mazao mengi
na kupunguza uhaba wa chakula Tanzania.
Kamwelwe
alisema Serikali inatambua umuhimu wa bonde hilo, ambapo katika
maandalizi ya uendelezaji wa bonde hilo upembuzi wa awali ulifanyika
kati ya mwaka 2013 na 2014.
Alisema
walibaini uwezekano wa kujenga bwawa kubwa katika eneo la Kikonge kwa
ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kudhibiti mafuriko katika bonde la
mto Ruhuhu, kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa eneo la takribani hekta
4,000 na kufua umeme mkubwa utakaounganishwa kwenye gridi ya Taifa.
Alisema
kwa sasa serikali kwa kushirikiana na benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB), ipo katika hatua ya kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi
yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji.



Blogger Comment
Facebook Comment