Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe
ZITTO Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo ameonesha hofu ya kustawi kwa chama chake iwapo kauli ya Rais John Magufuli ya kuzuia mikutano itaendelea kusimamiwa, anaandika Faki Sosi.
Amesema, kuna kila sababu ya kuruhusu mikutano ya kisiasa nchi nzima na kwamba, hatua ya kuzuia mikutano hiyo inatia hofu ya kudhoofisha chama hicho.Bakari Licapo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalengo kwa niaba ya Zitto amesema, chama hicho kina hofu ya kudhoofika iwapo agizo la Rais Magufuli litaendelea kutekelezwa.
Licapo alitoa kauli hiyo jana kwenye ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam ambapo amesema, wao kama vijana wameamua kumwandikia barua Rais Magufuli kama ambavyo Zitto alivyowaelekeza.
“…tumeamua kumwandikia barua rais ili abatilishe agizo hilo na kuruhusu mikutano ya hadhara nje ya majimbo ya viongozi husika,” amesema.
Licapo amesema kuwa, endapo agizo hilo litaendelea kuwa hai, ACT-Wazalendo kitalazimika kufanya mikutano yake ndani ya Mkoa wa Kigoma pekee na kwamba, hatua hiyo haiwezi kukitanua chama hicho.
Akizungumia upande wa madiwani Licapo amesema kuwa, chama hicho kitalazimika kufanya mikutano yake katika kata 49 walizozipata katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana.
Kwa zaidi ya mara moja Rais Magufuli amekuwa akitoa agizo la kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa nje ya majimbo ama kata ambazo viongozi hao wamechaguliwa.
Hatua hiyo imeelezwa na wachambuzi, wanasiasa na kada zingine kwamba, ni uvunjifu wa Katiba ya Tanzania na unyongaji wa demokrasia nchini.
0 comments :
Post a Comment