Makamu Wa Rais Akutana Na Mkurugenzi Mtendaji Wa Benki Ya Maendeleo Ya Afrika Anayeshughulikia Kanda Ya Afrika Mashariki

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeihakikishia Serikali kuwa itaendelea kuisaidia Tanzania katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo uimarishaji wa miundombinu ya barabara katika kuelekea kwenye Taifa la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Calleb Weggoro alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan 24-Aug-16 ofisini kwake, Ikulu, Dar es salaam.

Dkt. Weggoro alisema amefurahishwa na jinsi serikali inavyoshirikiana na sekta binafsi kupitia Mpango wa Ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na sekta za Umma (PPP) katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na anaamini ushirikiano huo utakuwa na manufaa kwa Taifa.

Mkurugenzi huyo alimweleza Mheshimiwa Makamu wa Rais  kuwa katika Mkakati wa Kitaifa wa 2016-2020 ulioandaliwa na Benki hiyo umeonesha maeneo matano mapya ambayo yatapewa kipaumbele katika kusaidia nchi za Afrika.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na masuala ya nishati, chakula, viwanda, utangamano wa nchi za Afrika na kuboresha maisha ya wananchi hasa vijana na wanawake kwa kuwawezesha kiuchumi kwa kuwapatia ajira.

Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais aliishukuru benki hiyo kwa misaada yake ambayo imeiwezesha serikali kutimiza azma yake ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake kwenye nyanja za kiuchumi na kijamii.

"Ni matumaini yangu kuwa katika huu mkakati mpya benki itakuwa tayari kuisadia Tanzania na nchi nyingine za kanda ya Afrika Mashariki, maana sote tunahitaji kusonga mbele kimaendeleo," alisema Mheshimiwa Samia.

Katika msafara huo Dkt. Weggoro alifuatana na Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo ya AfDB Tonia Kandiero ambaye alisema msaada wa benki hiyo katika kuimarisha miundombinu ya barabara ni jambo la msingi na akaelezea kufurahishwa kwake jinsi serikali inavyotekeleza miradi hiyo kwa ufanisi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia Kanda ya Afrika Mashariki  Dkt. Nyamajeje Calleb Weggoro,kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Bi.Tonia Kandiero, Ikulu jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia Kanda ya Afrika Mashariki  Dkt. Nyamajeje Calleb Weggoro mara baada ya kumaliza mazungumzo, Ikulu jijini Dar es salaam.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment