Waziri Mkuu Awataka Wakurugenzi Wasiwaondoe Walimu Wakuu Wasio na Shahada au Diploma badala yake wawahamasishe kwenda kusoma.


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa halmashauri na Maofisa Elimu nchini kutowaondoa katika nyadhifa zao Waratibu wa Elimu Kata na Wakuu wa shule za sekondari wasiokuwa na shahada, walimu wakuu wa shule za msingi wasiokuwa na diploma badala yake wawahamasishe kwenda kusoma.

“Maofisa Elimu na Wakurugenzi msije mkawaondoa wale walimu wakuu kwa zile sifa nilizosema bado muda ukifika tutatangaza.Msije mkawakurupusha sasa hivi waacheni waendelee na kazi zao tutatoa muda ili wajipange viziri,” aliema.

 Agosti 20 mwaka huu Waziri Mkuu alisema Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata na Wakuu wa shule za sekondari wanatakiwa kuwa na shahada huku walimu wakuu kwenye shule wanatakiwa kuwa na diploma.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini.

Alisema Mratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata ni lazima awe na shahada ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utolewaji wa elimu katika shule za sekondari na msingi.

“Wakuu wa shule za sekondari na waratibu wa elimu kata wasiokuwa na shahada wasiondolewe katika nafasi zao kabla ya kupewa nafasi ya kwenda kujiendeleza kwa masomo ili waweze kuwa na vigezo vya kuendelea kushika nyadhifa hizo,” alisema.

Alisema katika kuboresha maslahi ya walimu Serikali imetenga zaidi ya sh. bilioni tano kwa mwezi ambazo ni posho ya madaraka. Waratibu Elimu Kata wanapewa sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.

Waziri Mkuu alisema badala ya kuwaondoa kwenye nyadhifa hizo ni vema Wakurugenzi wakawahamasisha walimu hao kwenda kusoma ili na wao wanufaike na posho ya madaraka iliyoanza kutolewa na Serikali hivi karibuni.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka wazazi na walezi kwenda kuwaandisha watoto wenye umri wa miaka mitano katika shule za awali ambapo watapata fursa ya kujengewa msingi mzuri wa masomo kabla ya kuanza darasa la kwanza.

Pia aliagiza shule zote za msingi nchini zisizokuwa na madarasa ya awali kuhakikisha wanaanzisha madarasa hayo haraka na kuanza kutoa elimu hiyo.
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMIS, AGOSTI 25, 2016.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment