Baada ya kufutwa uanachama aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, Baraza Kuu la Uongozi CUF linatarajiwa kuanza kazi rasmi Ijumaa ya Septemba 30,2016.
Kabla ya Lipumba kurejea katika wadhifa wake wa Uenyekiti siku za hivi karibuni baada ya kujiudhuru mwaka jana, baraza hilo lilikuwa linakiongoza chama hicho.
Wanachama wa CUF wa mkoa wa Dar Es Salaam kwa kushirikiana na Wabunge wote wa CUF, wameandaa mapokezi makubwa siku ya Ijumaa kuanzia saa 2.00 asubuhi ambapo watawakaribisha Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa katika Ofisi Kuu za CUF Buguruni jijini Dar es Salaam.
Wajumbe hao walikuwepo Zanzibar kwenye Kikao Maalumu ambacho kililenga kutengeneza mustakabali muhimu wa chama hicho.
Mameya wa CUF, Madiwani, Kamati ya Uongozi ya Chama, Katibu Mkuu, Wakurugenzi, Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chama watawasili katika ofisini za chama hicho na kuanza kazi rasmi.