James Bwire, Meya wa Jiji la Mwanza
MGOGORO
umeibuka kati ya James Bwire, Meya wa Jiji la Mwanza na Kiomoni
Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji hilo kuhusu madai ya kutengenezwa madawati
8500 yanayodaiwa yapo chini ya kiwango, anaandikaMoses Mseti.
Meya Bwire, kwa muda mrefu amekuwa kwenye mgogoro na Adam Mgoyi, aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji hilo. Mgoyi kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Mvutano huo umeibuka baada ya Bwire kunukuliwa na gazeti moja la
kila siku kwamba, madawati yaliyotengenezwa na halmashauri hiyo yapo
chini ya kiwango na kwamba hayafai.
Hata hivyo, baada ya madai hayo, Kibamba ameibuka na kudai kuwa,
maelezo yaliyotolewa katika gazeti hilo (yakimnukuu Bwire) kwamba
madawati yapo chini ya kiwango sio kweli.
Kibamba jana amesema, baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa
madiwani wakidai kuwa wameigizwa mkenge, baadhi ya madiwani na wakuu wa
idara walikwenda kuyaangalia madawati hayo.
“Madiwani na baadhi ya watu wanasema kwamba mbao zilizotengeneza
madawati haya ni soft wood (mbao nyepesi) na sio hard wood (mbao ngumu),
sasa leo (juzi) waliamua kwenda `site` kuangalia na kujihakikishia kama
maelezo hayo ni ya kweli,” amesema Kibamba.
Kibamba amesema, baada ya madiwani hao kufika eneo husika
yanakotengenezwa madawati hayo, waliamua kuchukua baadhi ya madawati na
kuyapelekea kwa wataalamu wa misitu ambao anadai walijiridhisha ni
imara.
Kibamba ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amesema kuwa uongozi wa
jiji hilo upo makini katika kufuatilia kazi ya utengenezaji wa madawati
hayo na kwamba, hatakubali madawati yakitengenezwa chini ya kiwango.
“Mpaka sasa hivi tumetengeneza madawati 8500, yaliyobaki ni 900 na
hiyo yote ni kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa 2000 katika
shule zetu za umma na tumeamua kuanza kutengeneza madarasa kwanza,”
amesema Kibamba.
Hata hivyo, mtandao huu ulipomtafuta meya ofisini kwake kuzungumzia
suala hilo, alidai kwamba hana cha kuzungumza na kuwa, atafutwe
Elirehema Kaaya, Ofisa Mahusiano wa Jiji.
Kaaya alipoulizwa alisema, hawezi kuzungumza kwa kuwa bosi wake (mkurugenzi) tayari amelizungumzia suala hilo.
“Mimi sikatai kuzungumza ila kwa sababu bosi wangu tayari
kazungumza na kiitifaki, akizungumza bosi wako wewe (yeye) hauwezi
kuzungumza chochote na mimi ni mtaalamu wa itifaki,” amesema Kaaya.
Mmoja wa watumishi wa halmashauri hiyo, ambaye hakutaka jina lake
liandikwe gazetini, amesema kuwa anamshangaa meya huyo, kuibuka dakika
hizi za mwisho kudai madawati yapo chini ya kiwango.
“Yeye kipindi madawati haya yanatengenezwa, alikuwepo na huyu
mkurugenzi hakuwepo, kwanini hakuyasema hayo anayoyasema tangu zamani
kabla hayajaanza kutengenezwa labda kuna kitu hapo ,” amesema mtumishi
huyo.


0 comments :
Post a Comment