MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema,
amempongeza Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kwa
jitihada za kusuluhisha mgogoro wa uongozi uliokuwepo ndani ya Chama cha
Wananchi (Cuf).
Amewasihi viongozi wengine wa vyama vyote vya siasa nchini kuzingatia
Katiba za vyama vyao, misingi ya demokrasia na sheria za nchi, ili
kuepusha na kuondoa migogoro ndani ya vyama au kati ya chama kimoja na
kingine.
Amesema hakuna kiongozi wa kisiasa aliyekamilika kwa asilimia 100
kwakuwa , kila mmoja ana udhaifu wake. Mrema alitoa pongezi hizo jana
Dar es salaam kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari. Sehemu ya
taarifa hiyo ilisema, " TLP inampongeza Msajili na ofisi yake kwa
kutatua mgogoro huo kwa kuzingatia sheria za nchi, sheria ya vyama vya
siasa na pia, imezingatia misingi ya demokrasia ambayo ni nguzo ya mfumo
wa vyama vingi vya siasa".
Alisema chama hicho kinaamini kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa haikupendelea upande wowote kama baadhi ya watu wanavyodai, bali
imefanya kazi yake kwa kuzingatia sheria ya vyama vya siasa ambayo kwa
mujibu wa mamlaka aliyopewa Msajili na sheria hiyo kukifuta chama
chochote cha siasa nchini, endapo kitakwenda kinyume cha sheria hiyo,
pamoja na kusuluhisha migogoro.
Alisema kwa vile ofisi ya Msajili imeshatoa maelekezo kwa chama cha
Cuf, ni vyema wanachama wote wa chama hicho wakatulia na kutekeleza
maagizo yaliyotolewa na ofisi hiyo, ili kupata suluhisho la kudumu kwa
manufaa ya chama chao na kwa manufaa ya taifa.


0 comments :
Post a Comment