Aidha amesema atampokea
Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad siku atakapofika
kwenye ofisi hiyo makao makuu Buguruni kwa ajili ya kuandaa mikakati ya
kukijenga chama hicho. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini
Dar es Salaam, Profesa Lipumba alisema kikao cha Baraza Kuu la Uongozi
Taifa kilichofanyika Zanzibar ni batili kwa kuwa walikiuka katiba ya
chama hicho. Profesa
Lipumba alisema, kwa mujibu wa kifungu cha 79(2)(a) cha katiba ya chama
hicho kinasema kuwa, Mkutano Mkuu wa Taifa unaweza kuchukua hatua za
kinidhamu zozote zile, zikiwamo kumuachisha au kumkufukuza uongozi au
uanachama au yote mawili Mwenyekiti wa chama hicho.
Alisema kutokana na
kifungu hicho, “Mimi navuliwa uanachama na Mkutano Mkuu wa Taifa, sio
baraza la uongozi ambalo na lenyewe halijakidhi matakwa ya katiba ya
chama, kilichofanyika Zanzibar ni sawa na kikao cha harusi,” alisema.
Alisema pamoja na
kufanyika kwa kikao hicho, lakini pia idadi ya wajumbe waliohudhuria
kutoka Bara ni 9 ambao kati yao, watatu wajumbe wa kamati kuu na sita ni
wanachama wa kawaida, wakati Katiba ya chama hicho kinawataka kuwa na
wajumbe 22 kutoka Kamati Kuu ya chama.
Profesa Lipumba alisema,
katika katiba hiyo, pia kifungu cha 83(5) kinasema, baraza hilo
linaweza kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kutoa onyo kwa
maandishi, karipio kali.
Alisema, kabla ya
kufikia uamuzi huo, Katibu Mkuu alipaswa kuitisha Mkutano Mkuu ambao
pamoja na mambo mengine, ulitakiwa kumjadili ili wajumbe waweze kumpigia
kura ya kumwondoa. Pia alisema alipaswa kupewa nafasi ya kujieleza
katika mkutano mkuu ndipo wajumbe waamue hatua ya kumchukulia.
Kutokana na hayo alisema
yeye bado ni mwenyekiti halali na yupo ngangari katika kukijenga chama
na hafukuziki, hasusi wala hawezi kukihama chama hicho badala yake
amejiwekee mikakati ya kuhakikisha anawaunganisha wanachama wa chama
hicho.
Hata hivyo alisema
katika kipindi hiki ambacho chama hicho kimetoka kwenye mgogoro wa
uongozi uliosababisha Msajili wa vyama vya siasa kuingilia kati,
wanapaswa kukaa pamoja na kuondoa tofauti zilizopo ili waweze kukijenga
chama.
Katika hatua nyingine,
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema jana kuwa, haijapokea
mabadiliko yoyote ya uongozi kutoka katika chama hicho, hivyo
wanaendelea kumtambua Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama
hicho.
Aidha, ofisi hiyo ya
msajili wa vyama vya siasa imesema msimamo wake upo pale pale kwamba
Lipumba ni Mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho
mpaka hapo itakapoelezwa tofauti kwa kusimamia sheria za vyama vya siasa
na Katiba ya chama hicho.
Hivi karibuni Msajili wa
Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliwaeleza waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam kuwa msimamo wa msajili ni kwamba bado Lipumba ni
Mwenyekiti halali wa CUF na wanachama wote waliofukuzwa uanachama na
kikao cha Baraza Kuu la Uongozi cha Agosti 28 mwaka huu ni halali.
Alitoa angalizo kuwa,
kamati iliyoundwa kuongoza chama na viongozi walioteuliwa si halali na
kwa kuwa kifungu cha 8B (2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258
kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye si kiongozi wa chama haruhusiwi kufanya
kazi za chama kama viongozi, ofisi yake haiwatambui viongozi hao.
Chanzo-Habarileo


0 comments :
Post a Comment